Pages

Friday, September 27, 2013

Madiwani Bagamoyo waishukia Tasaf..watumikisha wananchi kazi za miradi mbalimbali huku fedha wakichukua wao.

Habari na Zawadi Chogogwe wa Tanzania Daima.
MADIWANI wa Halmashauri ya Bagamoyo, mkoani Pwani, wamelaani kitendo cha Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kufika katika vijiji vya Bagamoyo na kuwatumikisha wananchi kazi za miradi mbalimbali huku fedha wakichukua wao.

Madiwani hao waliibua hayo mjini Bagamoyo juzi katika kikao cha baraza la madiwani cha robo ya nne ya mwaka 2012 na 2013 kilichofanyika katika ofisi za mkurugenzi wa halmashauri hiyo ambacho kilihudhuriwa na wataalamu mbalimbali.

Diwani wa Kilomo, Hassan Usinga, alisema Tasaf wamekuwa na tabia ya kutofika kwa watendaji wa vijiji pindi wanapofanya kazi zao za miradi na badala yake wanaenda moja kwa moja kwa wanakijiji na kuwatumikisha katika miradi ya maendeleo huku wakiwalipa fedha kidogo.

“Kitendo cha kwenda kwa wanakijiji kuwafanyisha kazi na kuwalipa fedha kidogo kumechangia miradi mingi kuwa mibovu huku mingine ikiwa imekufa kama vile miradi ya kuku,” alisema Usinga.

Alisema taarifa za maendeleo ya vijiji zinaonyesha kuwa dawa za mifugo na matumizi zimetolewa kwa wanakijiji na kueleza kuwa taarifa hizo zikiwa hazina ukweli.

“Kutowashirikisha watendaji wa vijiji katika mikutano ya maendeleo kumepelekea kukosa wanakijiji wengi kushiriki katika mikutano yao,” alisema.

Alisema wanaoshiriki wanakuwa wachache hali inayowafanya Tasaf kuwavalisha fulana na kofia huku wakiwapiga picha na kuzipeleka kwa wafadhili kwa kuonyesha ushahidi kuwa wanakijiji wameshiriki mkutano huo wakati sio kweli.

Aliongeza kusema sh milioni 27 zilitengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara za 
 Tukamisasa kwenda Mbuyu, katika kata ya Ubena lakini cha kushangaza barabara hiyo haijajengwa kwa kiwango kutokana na wananchi kulazimika kuitengeneza kwa majembe baada ya kuona hakuna juhudi zozote za mamlaka husika.

“Tunaiomba Tasaf iache kutuchezea mchezo mchafu sisi watu wa Bagamoyo kwa kuwatumia wanavijiji kwa manufaa yao wenyewe,” alisema.
Wakati huohuo, madiwani hao walilalamika kuwa watumishi wa halmashauri hiyo hawana nyumba za kuishi za kiofisi, hali inayowafanya waishi katika nyumba za kupanga.

Akizungumza katika kikao hicho, Diwani wa Fukayosi, Ally Issa, alisema inatia aibu kuona watumishi wa Halmashauri ya Bagamoyo wakiishi katika nyumba za kupanga badala ya nyumba za kiofisi.

“Halmashauri inakusanya mamilioni ya fedha lakini inashindwa kuwajengea watumishi wake nyumba za kuishi. Mkurugenzi acha mambo ya siasa tunachotaka ni kuona nyumba za watumishi zinajengwa na kukabidhiwa,” alisema Issa.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Samwel Sariaga, alisema katika bajeti ya mwaka huu watajenga nyumba nne za watumishi ambazo kila moja itagharimu sh milioni 40.

Katika hatua nyingine, madiwani hao wametishia kuiburuza Bima ya Afya mahakamani, kwa kitendo cha kuwakata asilimia 5 kila mwezi ndani ya miaka mitatu bila kuwapatia kadi za matibabu.

Diwani wa Viti Maalum, Hapsa Jumam, alisema wakati wanaingia madarakani waliahidiwa watapewa kadi za matibabu, lakini cha kushangaza mpaka sasa hawajapewa.

No comments:

Post a Comment