SIKU moja baada ya serikali kufuta matokeo ya mtihani wa kidato
cha nne na kuamuru yaandaliwe upya, Mwenyekiti wa Chama cha
NCCR-Mageuzi, James Mbatia, ametaka wazazi wa wanafunzi waliojinyonga
kwa matokeo hayo walipwe fidia.
Wakati akitaka wanafunzi hao walipwe fidia, pia Mbatia alimshangaa
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, akihoji
anasubiri nini kung’atuka wakati kuna wanafunzi wamepoteza maisha kwa
uzembe wao.
Alisema Kawambwa anapaswa kujiuzulu kwani Katibu Mkuu wa Baraza la
Mitihani nchini, Joyce Ndalichako, hawezi kufanya mabadiliko makubwa ya
aina hiyo bila kuishirikisha wizara.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Mbatia ambaye pia
ni Mbunge wa kuteuliwa alisema serikali imekuja na majibu rahisi kwenye
jambo gumu, kwani uamuzi wa kufuta na kuandaa upya matokeo hayo kwa
utaratibu wa mwaka 2011, hauleti ufumbuzi wa mfumo wa elimu.
“Tume imekuja na majibu mepesi sana kwenye tatizo kubwa. Wanafunzi
wamejiua kwa msongo wa mawazo, wengine wamekata tamaa na kuamua kuolewa,
wengine kupata ujauzito, leo kwa uzembe wao wanataka kuwafaulisha
wanafunzi ili kupata sifa kisiasa, haiwezekani,” alisema.
Akichambua maoni ya tume hiyo, alisema imeibua hoja ambazo yeye
aliziwasilisha bungeni kupitia hoja yake binafsi ambayo ilizimwa na
wabunge wa CCM kwa sababu za kulinda masilahi ya chama chao.
Bofya chini kuendelea kusoma..
Alilishambulia Bunge kuwa limekuwa chanzo cha matatizo mengi kutokana na ubinafsi wa vyama bila kujali masilahi ya taifa.
“Bunge linaangamiza taifa kwa sababu ya itikadi. Hizi itikadi za vyama
zinaliangamiza taifa. Kuna umimi, ubinafsi kwenye mambo ya masilahi ya
taifa. Nawataka wabunge watoke usingizini,” alisema Mbatia.
Juzi serikali ilitangaza kufuta matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2012 na kuagiza yaandaliwe upya.
Uamuzi huo mgumu ulitangazwa bungeni na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.
Akisoma tamko hilo kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Lukuvi
alisema uamuzi huo wa serikali umetokana na mapendekezo ya tume ya
waziri mkuu iliyoundwa kuchunguza chanzo cha matokeo ya kidato cha nne
mwaka jana kuporomoka kwa kiwango cha kutisha.
Matokeo ya mitihani ya kidato cha nne mwaka 2012 yalionesha kuwa
kiwango cha ufaulu kimeshuka kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na miaka
ya hivi karibuni.
Matokeo yaliyotangazwa hivi karibuni, yalionesha kwamba kati ya
wanafunzi 367,756 waliofanya mtihani huo, watahiniwa 126,847 ndio
waliofaulu.
Katika idadi hii, wanafunzi waliofaulu katika daraja la kwanza hadi la
tatu ni 23,520, sawa na asilimia 6.4 na daraja la nne ni 103,327, sawa
na asilimia 28.1.
Watahiniwa 240,909, sawa na asilimia 65.5 ya wanafunzi wote,
waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2012, walipata daraja sifuri.
BAVICHA nao wanena
Lucy Ngowi anaripoti kuwa, Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA),
limemtaka Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa na
wasaidizi wake kujiuzulu mara moja ili kupisha wenye uwezo wa kusimamia
sekta hiyo.
Katibu Mkuu wa BAVICHA, Deogratias Munishi, alisema hayo katika tamko
alilolitoa jana baada ya Tume ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutoa
ripoti ya awali kuhusu sakata la kufeli vibaya kwa wanafunzi waliofanya
mtihani wa kidato cha nne mwaka jana.
Akinukuu moja ya sababu za kushindwa kwa wanafunzi hao, Munishi
alisema ni kutumika kwa alama mpya tofauti na miaka ya nyuma bila
taarifa kwa walengwa.
Alisema kuwa huo ni muendelezo wa siasa na mzaha kwa Watanzania kunakofanywa na serikali ya CCM kwenye masuala nyeti.
“BAVICHA inasisitiza Waziri Kawambwa na wasaidizi wake wajiuzulu
nyadhifa zao ili kupisha watu wenye uwezo wa kusimamia sekta hii na
taasisi zilizo chini yake,” alisema Munishi.
Aliongeza kuwa viwango hivyo vipya vilivyowekwa na Baraza la Mitihani
bila kushirikisha wadau ni kiashiria cha uzembe uliokithiri.
“Kama Baraza lilifanya maamuzi hayo bila waziri kujua nako kunaashiria
uzembe uliobobea wa waziri huyu wa kushindwa kujua kinachofanyika na
taasisi zilizo chini yake na kwa maana hiyo ni mzigo kwa taifa,”
alisema.
Kwa mujibu wa Munishi, suala hilo limeleta athari kwa wanafunzi, kwani baadhi yao wamepoteza maisha kwa kujinyonga.
No comments:
Post a Comment