VITU vilivyoporwa na watu wasiojuliana katika ajali ya msanii
mahiri wa filamu na muziki wa kizazi kipya nchini, Marehemu Hussein
Mkieti ‘Sharo Milionea’ eneo la Songa Kibaoni wilayani Muheza mkoani
Tanga, vimesalimishwa na wananchi wanaosadikiwa ni wezi.
Ajali hiyo ilitokea Jumatano iliyopita eneo hilo majira ya saa 2:30
nusu usiku, baada ya gari alilokuwa akiliendesha msanii huyo, Toyota
Harrier kuacha barabara na kuingia porini likigonga mti kisha kupinduka
na kumsababishia mauti.
Msanii huyo alikuwa akitokea jijini Dar es Salaam kuelekea kijijini
kwao Lusanga Muheza kwa ajili wa kuwasalimia wazazi wake pamoja na
kuwapelekea fedha za matumizi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe, jana
alithibitisha kupatikana vitu hivyo, ambako alisema upatikanaji wake
ulitokana na msako mkali uliofanywa na uongozi wa serikali Muheza
wakishirikiana na Jeshi la Polisi wilayani humo.
Kamanda Massawe alisema, baada ya kutokea kwa tukio hilo, Jeshi la
Polisi mkoani Tanga, liliweka mtego na kutangaza kuinunua simu ya
mkononi ya msanii huyo aina ya ‘blackberry’ ndipo moja kati ya
wanaodaiwa vibaka waliohusika kwenye tukio hilo, alipojitokeza na
kuipeleka kwa ajili ya kuiuza.
Alisema, wakati walipofika eneo ambalo walikubaliana, walikabidhi simu
hiyo kwa ajili ya kuikagua, lakini baadaye wezi hao walishtukia mtego
huo na kukimbia huku wakiiacha simu hiyo.
Aidha, Kamanda Massawe alivitaja vitu ambavyo vimesalimishwa kwa jeshi
hilo kuwa ni simu ya mkononi aina ya blackberry, Betri la gari, tairi
la akiba, radio ya gari, begi ambalo lilikuwa na nguo za marehemu, saa
ya mkononi na nguo ambazo alikuwa amevuliwa na vibaka wa eneo hilo mara
baada ya kutokea ajali hiyo.
Aliongeza kuwa, msako unaendelea na wamebaini baadhi ya washukiwa wa
uhalifu huo wamezikimbia nyumba zao kwa hofu ya kukamatwa.
Alisema, hadi sasa hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa na Polisi
kuhusiana na tukio hilo la uporaji na uchunguzi wa kuwabaini waporaji
ili waweze kutiwa mbaroni na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria
unaendelea, huku akitoa wito kwa wananchi kuacha kufanya vitendo vya
uporaji pindi ajali zinapotokea katika maeneo yao.
"Tupo kwenye uchunguzi mkali ili kuhakikisha tuwatia mbaroni wale wote
ambao waliohusika na kitendo cha kinyama alichofanyiwa msanii huyo,”
alisema Kamanda Massawe.Via Tanzania Daima.
No comments:
Post a Comment