Stori: Oscar NdaukaNI kweli ajali haina kinga! Nyota wa nyimbo za Injili Bongo, Bahati Lusako Bukuku ameumia mgongo na maeneo kadhaa ya mwili (nusu kifo) kiasi cha kushindwa kukaa, kusimama wala kutembea kufuatia ajali mbaya ya gari iliyotokea kwenye eneo la Ranchi ya Narco wilayani Kongwa, Dodoma saa tisa usiku wa kuamkia Jumamosi, Ijumaa Wikienda lina undani wa mkasa mzima.
Kwa mujibu wa chanzo makini, katika ajali hiyo ambayo Bahati alikuwa akienda Kahama, Shinyanga kwenye mkutano wa Injili, dereva wa gari alilokuwa akisafiria aina ya Toyota Nadia lenye namba za usajili IT 7945, Edison Mwakabungu ‘Eddy’ (31) aliumia sana kwenye vidole vya miguu na hawezi kutembea.
Wengine waliokuwemo kwenye ajali hiyo ni wacheza shoo wa Bahati, Frank Muha (20) na mwenzake ambaye jina lake halikupatikana mara moja.













