VITENDO vya wananchi kujichukulia sheria mikononi vinaendelea
kushika kasi ambapo askari wawili wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Ngara
mkoani Kagera, wanadaiwa kuuwa na wananchi wenye hasira kali jana.
Taarifa ambazo zililifikia Tanzania Daima Jumapili wakati tukielekea
mitamboni jioni, zilisema kuwa mauaji hayo yalifanyika baada ya wananchi
hao kuvamia na kukichoma moto kituo cha polisi cha Mugoma wilayani humo
baada ya askari hao kudaiwa kumpiga risasi fundi wa pikipiki.
Kwa mujibu wa mashuhuda, tukio hilo lilitokea mchana wakati askari
kadhaa wa kitengo cha usalama barabarani walipofika kwa fundi pikipiki
huyo na kutaka kuichukua pikipiki aliyokuwa akiitengeneza kwa madai kuwa
ilikuwa na makosa.
Kwamba fundi huyo aligoma na kueleza kuwa asubiriwe mwenye pikipiki ili kuepuka kudaiwa chombo hicho cha usafiri.
Mmoja wa mashuhuda hao, aliyatambulika kwa jina moja la Libela, alidai
kuwa baada ya mvutano wa muda mfupi, askari hao walifyatua risasi na
kumpiga fundi huyo mguuni na kifuani, hivyo kusababisha kifo chake.
Aliongeza kuwa, tukio hilo liliwapandisha hasira wananchi na kuwafukuza askari hao waliokimbilia katika kituo hicho cha polisi.
Lebela alifafanua kuwa, wananchi hao waliamua kukichoma moto kituo hicho
hatua iliyosababisha askari waliokuwemo kutoka na kukimbia kila mmoja
na muelekeo wake.
Alisema kuwa askari aliyetajwa kwa jina la Koplo Paschal alianguka
wakati akijinusuru, hivyo kuvamiwa na wananchi waliokuwa na zana
mbalimbali za jadi ambazo walitumia kumshambulia na kumuua papo hapo.
Wananchi hao pia wanadaiwa kumfuata askari mwingine anayetajwa kwa jina
la Pc Alex aliyekuwa amekimbilia kwenye nyumba ya mwananchi mmoja na
kumtoa kwa nguvu na kisha kuanza kumshambulia hadi kumuua.
Tukio hilo limetokea ikiwa ni siku ya soko katika eneo hilo la Mugoma
linalopakana na nchi jirani ya Burundi ambapo raia wa Tanzania na
Burundi hukutana na kufanya biashara jirani na kituo hicho cha polisi.
Kutokana na kuchomwa moto kwa kituo hicho, nyaraka mbalimbali zinadaiwa
kuteketea, huku pikipiki na baiskeli kadhaa zilizokuwa kituoni hapo nazo
zikiteketea.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Philip Kalangi, hakuweza kupatikana
kuthibitisha tukio hilo kutokana na simu yake ya kiganjani kuita bila
kupokelewa.Via TANZANIA DAIMA.
No comments:
Post a Comment