HATIMAYE Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana ilimpa masharti
matano ya dhamana msanii wa filamu nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’,
anayekabiliwa na kesi ya kuua bila kukusudia aliyekuwa msanii mwenzake,
Steven Kanumba.
Masharti hayo yaliyolewa na Jaji Zainabu Mruke, muda mfupi baada ya
mawakili wa Lulu, Peter Kibatara, Kennedy Fungamtama na Fulgence
Massawe, kuiomba mahakama hiyo impatie dhamana mteja wao ambaye amekuwa
akisota rumande tangu Aprili mwaka jana.
Mawakili hao walieleza kuwa
ombi la dhamana wameliwasilisha chini ya kifungu cha 148(1), (2) Cha
Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 .
Jaji Mruke alisema, ili mahakama impatie dhamana msanii huyo, ni
lazima asalimishe kwa Msajili wa Mahakama hiyo hati ya kusafiria,
kutotoka nje ya Dar es Salaam bila ruhusa ya mahakama, kuripoti kwa
msajili kila mwezi, kuwa na wadhamini wawili watumishi wa serikali,
ambao watasaini bondi ya sh milioni 20 kila mmoja.
Baada ya jaji huyo kutangaza masharti hayo, Lulu na wakili wake
walitoka nje ya ukumbi uliokuwa ukiendeshwa shauri hilo kwa ajili ya
kwenda kwa msajili kutimiza masharti hayo, lakini bahati mbaya hakuwepo
ofisini, hivyo kumfanya Lulu kurudishwa rumande hadi leo, atakapoletwa
kwa ajili ya kutimiza masharti hayo mbele ya msajili wa mahakama hiyo.
Licha ya mahakama hiyo kumpatia masharti ya dhamana Lulu, kutokana na
ombi lake Na.125/2012, lakini bado kesi ya msingi inayomkabili, ambayo
ni ya kuua bila kukusudia, haijapangiwa jaji wala tarehe ya kuanza
kusikilizwa.
Desemba 21, mwaka jana, Hakimu Mkazi Christine Mbando wa Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu aliifunga kesi ya kuua bila kukusudia ya Lulu na
kuihamishia rasmi Mahakama Kuu na uamuzi huo ulitokana na upande wa
jamhuri kumsomea maelezo ya kesi yake kwa kina na kuieleza mahakama kuwa
wanakusudia kuleta jumla ya mashahidi tisa.
No comments:
Post a Comment