Wamo pia wafanyabiashara wakidaiwa kushiriki mauaji
JESHI la Polisi katika mikoa ya Iringa na Mbeya, limewakamata
watu 29 wakiwemo askari wawili wanaotuhumiwa kuwa majambazi hatari
waliohusika na matukio ya mauaji na uporaji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman, aliwaambia waandishi
wa habari kuwa miongoni mwa waliokamatwa ni askari Samuel Balumwina
(31) mwenye namba MT 85393 kutoka kikosi cha JKT Itende (844KJ) na PC
Samuel Kigunye (27) namba G.9101.
Askari hao wanatuhumiwa kuazimisha sare za majeshi hayo kwa majambazi.
Na kuongeza kuwa polisi atashtakiwa kijeshi na kuunganishwa na wengine
kwa makosa ya mauaji na uporaji wa mali.
Watuhumiwa hao wa ujambazi wanadaiwa kuhusika katika matukio makubwa
likiwemo la mauaji ya askari polisi G 68 PC Japhary aliyepigwa risasi
ubavuni akiendesha gari la namba PT 0665 lilipokuwa doria Mkwajuni,
wilayani Chunya.
Athuman alisema wananchi wa eneo la Mkwajuni wilaya ya Chunya wakiwa
na silaha za jadi kwa hasira ya kuuawa kwa askari Japhary,
walimshambulia dereva wa gari la majambazi Shaban John (33) ambaye kabla
hajafa aliwataja wenzake alioshirikiana nao.
Alisema uporaji huo waliufanya katika kituo cha mafuta cha Matundasi ambapo walipora kiasi cha sh milioni 2.2.
Kamanda Athuman aliwataja watuhumiwa waliomuua PC Japhary kuwa ni
Master, Emmanuel Mdendemi, Mashaka Hongole, Manase Kibona, Mashaka
George, John Mahenge (39) na Norasco Mabiki(32) ambao licha ya
kutuhumiwa kwa mauaji pia wameshiriki katika uporaji kwa kutumia silaha
kwa masista eneo la Wanging’ombe, mkoa wa Njombe.
“Mtandao wa watuhumiwa hawa ni wa hatari sana na unaungana na wale
kutoka mikoa ya Iringa na Dar es Salaam,” alisema na kuongeza kuwa watu
hao pia wanatuhumiwa kuteka na kuwaua Festo Afwilile Kyando (45) mmiliki
wa gari lenye namba T586 AGX aina ya Mitsubishi Fuso na utingo wake,
Jamali Msangu (26) na miili yao kutupwa porini Februari 2, mwaka huu.
Alitaja watuhumiwa waliowateka, kuwaua na kisha kupora mali kuwa ni
Rajabu Mbilinyi (25) mkazi wa jijini Dar es Salaam, Gregory Charles
(25), mkazi wa Sabasaba Mbeya na Ghati Mbilinyi (32) mkazi wa Mwanjelwa
ambaye inadaiwa gari lake lenye namba za usajili T464 BLX aina ya Noah
ndilo lililotumika kufanya mauaji na alikuwa akitumia sare za Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na zile za polisi.
Wengine ni Japhet Ng’ang’ana (24) mkazi wa Makambako anayedaiwa
kutunza silaha zilizokamatwa na mfanyabiashara wa Makambako na ndugu
wawili Hilary Ng’ang’ana (30) na Claud Ng’ang’ana (36) wakazi wa
Nyololo, Mafinga wakishirikiana na Francis Sanga (30) mkazi wa Tunduma
anayetuhumiwa kupokea mali za wizi baada ya mauaji ya Mafinga.
Silaha zilizokamatwa zikidaiwa kutumika katika matukio ya ujambazi ni
bunduki aina ya shortgun iliyofutwa namba, gobore moja lililokamatwa
kwenye gari la Gathi Mbilinyi T464 BLX Noah na bastola tatu
zilizotengenezwa kienyeji zinazotumia risasi za shortgun zilikamatwa
Makambako na Mbeya kwa Hilary.
Polisi pia imekamata risasi 155 zikiwemo 31 za SMG/SAR na 99 za short
gun na 25 za bastola, magari matano na sare za majeshi zinazotumiwa
kwenye vitendo vya ujambazi.
Kamanda Athuman alisema majambazi tisa waliohusika na mauaji ya
Mafinga watasafirishwa chini ya ulinzi mkali kwenda mkoani humo ili
kufikishwa mahakamani.
No comments:
Post a Comment