Young Africans imetoka sare ya bao 1-1 dhidi ya timu ya Mtibwa Sugar
kutoka Morogoro katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom uliofanyika leo
jioni katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Katika mchezo wa leo Young Africans imeshindwa kuondoka na ushindi
kutokana na washambuliaji kushindwa kutumia nafasi nyingi za wazi hali
iliyopelekea mchezo kuwa mgumu kwa kipindi chote cha mchezo.
Didier
Kavumbagu na Jerson Tegete walikosa nafasi za mabao ya wazi zaidi ya
tano katika kipindi cha kwanza, kwani umahiri wa mlinda mlango Sharrif
Cassilas wa mtibwa uliweza kuwafanya waonekane bora muda wote wa
mchezo.
Dakika ya 45, Shaban Kisiga aliipatia Mtibwa Sugar bao la
kwanza kwa kichwa akimalizia mpira wa kona uliopigwa na Said Mkopi na
mpira huo kumkuta mfungaji akiwa peke yake na kuukwamisha mpira kwa
kichwa.
Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, Young Africans 0 - 1 Mtibwa Sugar.
Kipindi
cha pili kilianza kwa Young Africans kufanya mbadiliko ambapo Said
Bahunuzi, Hamis Kiiza na Nurdin Bakari waliingia kuchukua nafasi za
Frank Domayo, Didier Kavumbagu na Athumani Idd.
Mbadiliko hayo
yaliongeza uwezo wa kumiliki mpira kwa timu ya Young Africans kwani eneo
la kiungo walilitawala vizuri hali iliyoplelekea kufanya mashambulizi
mengi langoni mwa Mtibwa Sugar lakini umakini wa washambuliaji bado
ulikua ni tatizo.
Hamis Kiiza
aliipatia Young Africans bao la kusawazisha dakika ya 86 akimaliza shuti
kali lilopigwa na Said Bahanuzi kutoka upande wa kulia na kumkuta Kiiza
aliyeukwamisha mpira huo wavuni na kuwa bao la kusawazisha.
Young
Africans ilikosa tena mabao ya wazi dakika za lala salama kupitia kwa
washambuliaji wake Tegete, Msuva, Kiiza na Bahanuzi ambao walikosa mabao
hayo hali iliyopelekea wapenzi na wanachama wa Young Africans kukosa
raha kutokana na nafasi hizo.
Mpaka mwisho wa mchezo Young Africans 1- 1 Mtibwa Sugar.
Kocha
Mkuu wa Young Africans Ernest Brandts amesema kikosi chake hakikucheza
vizuri katika mchezo wa leo, wachezaji walipata nafasi nyingi za wazi
lakini hawakuwa makini hali hiyo ndio iliyopelekea mchezo kuisha sare ya
mabao 1-1.
Young Africans: 1.Ally Mustafa
'Barthez', 2.Mbuyu Twite, 3.Oscar Joshua, 4.Nadir Haroub 'Cannavaro',
5.Kelvin Yondani, 6.Athumani Idd/Nurdin Bakari, 7.Saimon Msuva, 8.Frank
Domayo/Said Bahanunzi, 9.Didier Kavumbagu/Hamis Kiiza, 10.Jerson Tegete,
11.Haruna Niyonzima
Mtibwa Sugar: 1.Hussein
Sharrif, 2.Said Mkopi,3.Issa Rashid, 4.Rajab Mihamed, 5.Salum Sued,
6.Shaban Nditi, 7.Vicent Barnabas, 8.Rashid Gumbo, 9.Hussein Javu,
10.Shaban Kisiga, 11.Ally Mohamed
No comments:
Post a Comment