MWANAMKE asiyefahamika juzi alimtelekeza mtoto mdogo wa kike
anayekadiriwa kuwa na miaka mitano ambaye ni mgonjwa katika eneo la
Kivuko cha Kisorya, wilayani Bunda, Mara.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kisorya, Mashaka Mahulilo, alisema mtoto
huyo ambaye pia amepooza mguu mmoja alitelekezwa juzi, majira ya saa
9:30 mchana katika eneo la kijiji cha
Kisoya, baada ya Kivuko cha MV
Ujenzi kinachofanya safari kati ya ng’ambo ya Kisorya, wilayani Bunda,
na Ngoma Lugezi wilayani Ukerewe kutia nanga katika eneo hilo.
Alisema mwanamke huyo alikuwa ni kati ya abiria waliokuwa ndani ya
kivuko hicho wakitokea wilayani Ukerewe na kwamba baada ya kufika eneo
hilo alimtelekeza mtoto huyo.
Mahulilo alisema mtoto huyo ambaye ni kiziwi aliachwa na mama yake
eneo hilo, akiwa na mifuko miwili midogo ya nailoni iliyokuwa na nguo
zake.
Alisema mtoto huyo aliokotwa na wasamaria wema akiwa ukingoni mwa
daraja la kivuko hicho na kwamba alichukuliwa na mwananchi mmoja mkazi
wa kijiji hicho aliyekabidhiwa mbele ya viongozi wa serikali ambaye sasa
ndiye anayeishi naye.
Kutokana na tukio hilo, baadhi ya wananchi wamelaani kitendo kilichofanywa na mwanamke huyo.
No comments:
Post a Comment