Dar es Salaam.
Watu zaidi ya 40 wanahofiwa kufukiwa na kifusi
baada ya jengo la ghorofa 16 lililokuwa linajengwa kuporomoka katikati
ya Jiji la Dar es Salaam jana asubuhi.
Kuporomoka kwa ghorofa hilo lililokuwa katika Mtaa
wa Indira Gandhi, kulizua huzuni, taharuki na simanzi kwa ndugu na
jamaa waliofika kwenye eneo la tukio kutaka kufahamu nini kimetokea.
Shughuli mbalimbali katikati ya jiji hilo zilisimama kwa siku nzima baada ya jengo hilo kuanguka na kusababisha vifo vya watu watano, 13 kuokolewa huku zaidi ya watu 40 wakisadikiwa kufukiwa na kifusi cha udongo wa jengo hilo.
Jengo lililoporomoka
Jengo hilo lililokuwa likijengwa mkabala na
Msikiti wa Shia Ithnasheri ulioko Barabara ya
Indira Gandhi na Kampuni ya ‘Lucky Construction Limited’ lilianguka majira ya saa 2.30 asubuhi wakati ujenzi ukiendelea juu huku chini watoto wakicheza mpira na mama lishe wakiendelea na biashara zao kama kawaida.
Indira Gandhi na Kampuni ya ‘Lucky Construction Limited’ lilianguka majira ya saa 2.30 asubuhi wakati ujenzi ukiendelea juu huku chini watoto wakicheza mpira na mama lishe wakiendelea na biashara zao kama kawaida.
Pamoja na vifo na wengine kujeruhiwa, magari
takribani manne yalifunikwa na kifusi cha jengo hilo na kupondwa pondwa
na kuwa kama chapati.
Katibu wa Msikiti wa huo wa Shia Ithnasheri,
Mushtaq Damji alisema: “Leo tulikuwa na kitu kama jumuiya kwa jamii ya
wahindu, tulipanga kusherehekea lakini yote yakafutika.
“Baada ya swala ya alfajiri, watu walikuwa
wanazungumza hapa na pale na baada ya kupambazuka, watoto walikuwa
wanacheza mpira, walikuwa 9. Sasa, bahati nzuri watoto saba wakakimbia
na watoto wawili wakawa wamekwama,” alisema Damji.
Naye Mlinzi wa Msikiti huo, Athuman Nassor
alisema: “Mimi nafanya kazi ya ulinzi hapa msikitini, lakini nilikuwa
ninashangaa kiasi cha saruji kilichokuwa kikitumika kukorogea zege,
kweli walikuwa wanazidisha mchanga.
“Niliwahi kuwaambia hata hawa vibarua, kuwa hii
inayofanyika mbona siyo…,” alisema mlinzi huyo. Alisema; jana ilikuwa
siku ya kumwaga zege ghorofa ya 16 na kulikuwa na vibarua wapatao 50
ambao kila mmoja alikuwa na ndoo yake tayari kuanza kazi kabla ya
ghorofa hilo kuporomoka.
Mlinzi huyo alisema kuwa wakati tukio hilo linatokea alikuwa mbali kidogo na eneo la tukio na kusema kuwa bila shaka baadhi ya kinamama lishe ni miongoni mwa waliofukiwa.
Habari zilizopatikana baadaye jana jioni zilidai kuwa mmiliki wa
jengo, Ally Raza pamoja na mhandisi wa Kampuni iliyokuwa ikijenga jengo
hilo ya Lucky Construction Limited walidakwa kwenye Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere wakijiandaa kutimka.
Viongozi wamiminika
Rais Jakaya Kikwete alifika katika eneo la tukio
saa 6:45 mchana na alipata maelezo mafupi ya tukio hilo kutoka kwa Mkuu
wa Mkoa, Said Meck Sadik na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es
Salaam, Suleiman Kova.
Baada ya maelezo hayo, Rais Kikwete aliyetumia
dakika tisa, alimwambia Mkuu wa Mkoa na
Kamanda Kova: “…mmiliki na mhandisi lazima wakamatwe mara moja.”
Kamanda Kova: “…mmiliki na mhandisi lazima wakamatwe mara moja.”
Kikwete baadaye alitikisa kichwa kuonyesha masikitiko na kuondoka.
Viongozi wengine waliofika ni Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal ambaye hata hivyo hakuzungumza lolote hata baada ya kupata taarifa kutoka kwa mkuu wa mkoa.
Naye aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa (UN) ambaye sasa ni Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa
Kimataifa wa CCM, Dk Asha-Rose Migiro alisema tukio hilo linaumiza na
kusikitisha kwani limepoteza nguvu kazi ya taifa.
“Ni vigumu kupata maneno ambayo yatabeba uzito wa
tukio hili lakini wajenzi wanatakiwa kuwa makini na ujenzi wao,” alisema
Migiro.
Wananchi wajitokeza kuokoa
Mapema Wananchi waliojitokeza kwa kushirikiana na
askari polisi na mgambo wa Jiji walioanza kuondoa kifusi cha mchanga kwa
kutumia mikono kutokana na kutokuwapo kwa vifaa vya kuondolea kifusi
hicho.
Ilipofika saa 4.30 ndipo trekta (kijiko) moja lilifika na
kushirikiana na wananchi ingawa halikuweza kuhimili kazi hiyo nzito na
kuhitajika trekta maalumu la kubeba na si kuzolea ili kunusuru uwezekano
wa kuhatarisha uhai wa waliofukiwa na kifusi.
Naibu Meya wa Halmashauri ya Ilala, Kheri Kessy
alisema,mwaka 2007 walitoa kibali kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)
kwa kushirikiana na ‘Ali Raza Investment Limited’ kujenga jengo la
ghorofa 10.
“Kibali tulichotoa sisi ni cha kujenga ghorofa 10
na mkaguzi wetu alikuwa anafuatilia kila hatua hadi ilipofika ghorofa ya
10 akawa amemaliza kazi yake,” alisema Kessy.
Alipotakiwa kueleza kwanini hawakuchukua hatua
baada ya kuendelea kujengwa hadi kufikia ghorofa zaidi ya 16 alisema,
wao kwa hilo hawahusiki ila kuna taasisi zingine za Serikali
zinazosimamia majengo zinatakiwa kuulizwa.
“Kama nilivyosema,sisi tulitoa kibali cha kujenga
ghorofa 10 na mkaguzi wetu alikagua hadi ghorofa ya 10 hivyo kama
waliendelea kujenga sisi hatujui kwani kuna CRB (Bodi ya Usajili wa
Makandarasi) au ERB (Bodi ya Usajili ya Wahandisi) wao ndio wanahusika
zaidi watawaelezeni,” alisema Kessy.
NHC yatoa maelezo
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) jana lilitoa
taarifa yake kuhusu tukio hilo na kueleza kuwa mradi wa ujenzi wa
ghorofa hilo ulikuwa ukifanyika kwa ubia kati yake na Kampuni ya Ujenzi
ya Ladha ya jijini Dar es Salaam, ambapo NHC lilikuwa na ubia wa
asilimia 25.
Ilieleza kuwa mbia huyo alipaswa kabla ya kuanza
ujenzi kupata vibali kutoka kwenye mamlaka husika na kuwa na wataalam wa
ujenzi na washauri waliokubalika na kuthibitishwa na mamlaka husika,
kwani NHC ilitoa ardhi tu kwa ajili ya ujenzi huo na ubia ungekamilika
mara baada ya jengo hilo kumalizika kujengwa.
“Mbia akishapata wataalam hao yeye ndio
anayehusika kuingia nao mikataba ya kazi ya kujenga na kusimamia ubora
wa jengo husika kwa mujibu wa sheria” ilieleza taarifa hiyo.
Ilieleza kuwa NHC imesimamisha utoaji wa miradi
mipya ya ubia ili kuweza kutathimini mafanikio na changamoto za
utekelezaji wa miradi ya ubia na hivyo kuwezesha kutengeneza sera mpya.
Kamanda Kova azungumza
Naye Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova alithibitisha kutokea kwa vifo hivyo na majeruhi na
kuahidi kuwachukulia hatua kali waliosababisha tukio hilo.
Kamanda Kova alisema wanawashikilia watu watatu
kwa mahojiano ambao ni Mhandisi Mkuu, Mkaguzi Majengo na Mhandisi
Majengo wote wa Halmashauri ya Ilala kwa mahojiano zaidi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Said Meck Sadik amesema kuwa biola shaka kuporomoka kwa jingo hilo
kumesababishwa na uzembe.
“Huu ni uzembe kabisa…, kuna watu wamepewa kazi za
kusimamia ambao inaonyesha hawakufanya kazi zao ipasavyo. “Wote
waliohusika, tutawatafuta popote walipo na watatueleza…,” alisema.
Mkuu wa mkoa pia aliagiza kusitishwa kuendelea kwa
ujenzi wa jengo pacha kama hilo hadi uchunguzi wa kina utakapofanyika
kuona kama limetimiza vigezo.
Mtoto aliyenusurika anena
Mtoto mmoja aliyekuwa akicheza mpira na wenzake
katika eneo hilo, Ally Karim alisema walikuwa tisa wakicheza mpira mara
akaona jengo linadondoka na yeye akakimbia.
“Kati ya hao tisa ni mimi pekee ndiye nilikimbia
lakini wengine walifukiwa chini na watatu wameokolewa lakini wengine
wanne bado wako chini ya huo udongo…,” alisema Karim.
Kwa upande wake shuhuda wa tukio hilo, Chacha Boniface alisema jengo hilo lilikuwa na vibarua wengi juu wakiendelea na ujenzi.
“Vibarua walikuwa wengi, wengine walikuwa
wakichanganya kokoto, wengine wakijenga matofali na wengine wakipiga
plasta, bado mafundi wote wamefukiwa na kifusi,” alisema Boniface na
kuongeza:
“Achilia mbali hao vibarua na mafundi, chini kulikuwa na magari
yanapita, watoto wakicheza na mama ntilie (mama lishe) wakiuza uza chai
hivyo nafikiri si chini ya watu 40 wamefukiwa”.
Naye Idd Baka alisema gari yake aina ya Noah
ambayo aliiegesha katika eneo hilo na kushuka kwenda dukani kwa
manunuzi, ndani ya gari hilo alikuwamo mkewe na watoto wawili, nao pia
wamefunikwa na kifusi.
“Bado nawasiliana na mke wangu kwa njia ya simu,
(ilikuwa saa 8 mchana) kwani mimi nilishuka kwenda dukani kurudi
nikakuta kadhia hii, sijui itakuwaje” alisema Baka kwa huzuni.
Naye jirani wa jengo hilo, Ramesh Abdallah alisema alijua jengo hilo litabomoka kutokana na kujengwa chini ya viwango.
Alisema ndani ya miezi sita ilikuwa tayari ghorofa 12 zimekamilika kujengwa, hali ambayo aliitilia shaka uimara wake.
“Hata ukiangalia mchanga ni mwingi kuliko saruji,
angalia hata nondo zake si za kujengea ghorofa 16, hii ndio Tanzania na
wajanja ndio wanaofaidi huku watu wakipoteza maisha kizembe,” alisema
Abdallah.
Wanasiasa
Awali Mwenyekiti wa Chama Cha NCCR-Mageuzi James
Mbatia ambaye pia ni Mhandisi alitoa ushauri kubomoa kuta za msikiti na
kibanda kilichokuwa katikati ili kurahisisha uokoaji jambo ambalo
halikufanyika.
“Kama unavyoona nafasi ni ndogo, tunatakiwa
kuheshimu mawazo ya kila mmoja ambaye anakuwa na nia nzuri sasa angalia
matrekta (matatu) nafasi ndogo,” alisema Mbatia na kuongeza:
“Ujuzi wetu katika masuala ya uokoaji bado ni
mdogo, wamekuja Askari wa JKT, je, hawa askari kweli wanafundishwa
kupambana na majanga?” Alihoji Mbatia.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Julius
Mtatiro alisema kilichotokea ni matokeo ya rushwa na uzembe ndivyo
vilivysababisha jengo hilo kuporomoka.
“Kweli unataka kusema hili jengo lilikuwa
halikaguliwi? Kilichokuwa kikifanyika ni watu kula fedha bila kutekeleza
wajibu wao hivyo tutaendelea kuangamia kama watu hawatakuwa makini
katika sekta zao,” alisema Mtatiro.
Red Cross walia kukosa vifaa
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Msalaba Mwekundu
Mkoa wa Dar es Salaam, Hidan Ricco alisema kuwa kazi ya uokoaji ilikuwa
ngumu kwani walikosa vifaa madhubuti kwa kazi hiyo.
Alisema pia kuwa vifaa vilikuwa vya ‘kuungaunga’ kutoka taasisi mbalimbali ambavyo hata hivyo kwa kiasi fulani vilisaidia.
Alipoulizwa kuhusu ajali hiyo, Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi alisema sio kila mtu anazungumza
kuhusu tukio hilo na kusisitiza kuwa atafutwe Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Said Meck Sadik.
Naye Msajili Msaidizi wa Bodi ya Usajili wa
Wakandarasi (CRB), Flora Mwombeki ambaye alikuwa eneo la tukio jana
alisema bodi hiyo inautambua mradi wa ujenzi wa jengo hilo lililokuwa
likijengwa na Kampuni ya Lucky Construction Ltd.
“Mimi sio msemaji wa CRB ila mradi huu tunautambua, kuhusu nani
alikuwa mkandarasi siwezi kukujibu kwa kuwa sioni kibao kinachoonyesha
kuwa ni kampuni ya Lucky, nadhani baadaye ukiwatafuta wahusika wakuu
watakupa ufafanuzi,” alisema Mwombeki.
Matukio mengine
Hii ni mara ya pili kwa mwaka huu jengo kuanguka,
kwani Februari jengo la ghorofa nne lilianguka maeneo ya Kijitonyama
Mpakani jijini Dar es Salaam na kusababisha kifo cha mtoto wa miaka 9.
Licha ya ujenzi wa jengo hilo kusimamishwa miaka 10 iliyopita, familia ya marehemu iliendelea kuishi katika jengo hilo.
Juzi 21, 2008 jengo la ghorofa 10 lilikuwa
likiendelea kujengwa na Kampuni ya NK Decorators katika Mtaa wa Mtendeni
Kisutu jijini Dar es Salaam liliporomoka na kuua mtu mmoja.
Mwaka 2006 pia liliwahi kuporomoka jengo na kuua
mtu mmoja ambapo baada ya tukio hilo, tume ya kukagua majengo iliundwa
na aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, Edward Lowassa na ripoti yake
ilikabidhiwa serikalini lakini mpaka leo hii ripoti hiyo haijawahi
kutolewa hadharani.
Imeandikwa na Ibrahim Bakar, Ibrahim Yamola, Pamela Chilongola, Fidelis Butahe, Kelvin Matandiko, Aisha Ngoma, Aidan Mhando
No comments:
Post a Comment