RAIS Jakaya Kikwete ameomba msaada wa walimu wa Hisabati na
Sayansi kutoka nchini Jamaica ili kukabiliana na upungufu wa wataalam
hao nchini.
Rais Kikwete alitoa ombi hilo juzi kwenye Hotel ya Sheraton mjini
Addis Ababa, Ethiopia wakati wa mkutano wake na Waziri Mkuu wa Jamaica,
Mama Portia Simpson Miller.
Ikulu ilisema kuwa Rais Kikwete alikuwa Addis Ababa kuhudhuria
sherehe za miaka 50 tokea kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika, Juni 25, 1963
na Mkutano wa 21 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa AU wakati Mama Simpson
Miller alipokuwa mmoja wa viongozi mashuhuri wa nchi mbali mbali duniani
walioalikwa kuhudhuria sherehe hizo.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu iliyosambazwa jana kwa
vyombo vya habari, ilisema kuwa katika mazungumzo ya viongozi hao
wawili, Mama Portia Simpson Miller ambaye aliapishwa kuwa Waziri Mkuu wa
Jamaica Januari 5, 2012 baada ya chama chake cha Peoples National Party
(PNP) kushinda uchaguzi mkuu nchini humo, alimwuliza Rais Kikwete jinsi
gani Jamaica inavyoweza kuisaidia Tanzania.
Kutokana na swali hilo, Rais Kikwete aliomba mambo mawili, mosi
kupatiwa walimu wa masomo ya hisabati na sayansi pamoja na kocha wa
riadha.
“Mawili makubwa ambayo mnaweza kutusaidia, moja ni walimu wa hisabati
na masomo ya sayansi kama mnao wa kutosha na pia kocha wa riadha ili
tuweze kufufua upya mchezo huo ambao Tanzania ilikuwa inatamba nao
duniani katika miaka ya 1970,” alisema Rais Kikwete.
Kutokana na ombi hilo, mama huyo alimwahidi Rais Kikwete kuwa Jamaica ina uwezo wa kusaidia katika maeneo yote mawili.
“Hili la walimu tutaliangalia mara moja nikirejea nyumbani. Tutasaidia
kwa kadri inavyowezekana kwa sababu najua fika juhudi zako kubwa ambazo
umekuwa unafanya katika eneo hili la elimu na mafanikio makubwa ya
jitihada zako.”
Kutokana na makubaliano hayo, serikali sasa inatarajiwa kupata walimu
wa masomo hayo mawili na kocha wa mchezo wa riadhaa. Hata hivyo taarifa
hiyo haikutaja idadi ya walimu wa masomo hayo.
Katika matokeo ya kidato cha nne na sita, kumekuwa na idadi kubwa ya
wanafunzi wanaofeli masomo hayo kwa madai kuwa walimu wanaoweza
kufundisha masomo hayo ni wachache.
Lakini kibaya zaidi wataalam wa masomo hayo licha ya uchache wao,
hawana motisha na ndio sababu yao kutofundisha vizuri na kusababisha
matokeo mabaya katika masomo hayo.
Mbali ya makubaliano hayo, nchi hizo mbili zimeahidi kuongeza
ushirikiano katika nyanja mbalimbali na kuangalia uwezekano wa Tanzania
kufungua aina ya uwakilishi katika Kisiwa hicho cha Caribbean katika
miaka miwili ijayo.
Kuhusu kocha wa riadha, Mama Simpson Miller amesema kuwa na hilo
halina pingamizi kwa sababu yeye alikuwa Waziri wa Michezo kwa miaka
mingi na kuwa kwa sasa Wizara ya Michezo iko kwenye Ofisi yake ya Waziri
Mkuu.
“Nilikuwa waziri wa miaka mingi wa michezo katika nchi yangu na kwa
sababu ya umuhimu wa michezo, nimeamua kuiweka shughuli ya michezo
katika Ofisi yangu ya Waziri Mkuu.”
Jamaica ni moja ya nchi zinazoongoza katika mchezo wa riadha duniani
ikiwa imetoa wanariadha wengi mabingwa wa dunia akiwamo bingwa wa sasa
wa Olimpiki na dunia katika mbio fupi za mita 100 na 200, Usain Bolt.
No comments:
Post a Comment