KAMPUNI ya ACG-E-Bus Ticketing ya jijini Dar es Salaam imekuja
na huduma ya kukata tiketi za mabasi yaendayo mikoani kwa njia ya
mtandao wa simu za mkononi.
Huduma hiyo ambayo tayari imeshaanza, itakuwa dawa ya kuwaondoa wapiga
debe ambao mara nyingi wamekuwa wakilalamikiwa na abiria kwa usumbufu.
Akizungumza jana, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni
hiyo, Martin Kaswahili, alisema huduma itafanywa kupitia mitandao yote
ya simu za mkononi na itaondoa usumbufu wa abiria kulazimika kufika
Kituo cha Mabasi Ubungo kukata tiketi.
Kwa mujibu wa Kaswahili, kuanzishwa kwa huduma hiyo ni matokeo ya
utafiti wa muda mrefu katika vituo vya mabasi vya miji mikubwa ya
Ubungo, Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya ambao umebaini kuwapo kwa urasimu
na usumbufu wa abiria kupata tiketi za mabasi wanayotaka kusafiri nayo.
“Tulifanya utafiti katika sekta ya usafirishaji wa nchi kavu hasa
mabasi, tuliongea na wenye mabasi, baadhi ya mawakala, abiria wenyewe
na tukagundua tatizo kubwa la abiria waendao mikoani hasa katika vituo
vya miji mikubwa kama vile Mwanza, Dar es Salaam, Mbeya na mikoa
mingine ni urasimu wa kupata tiketi na abiria kusumbuliwa hivyo njia ya
mtandao ni suluhisho kwao,” alisema Kaswahili.
Kaswahili alisema huduma hiyo inapatikana kupitia mitandao ya simu za mikononi za Tigo, Airtel, Voda.
“Ili kupata huduma hiyo, abiria anatakiwa kupiga *150*16# kisha
utakuja ujumbe wa kukukaribisha E-Bus Ticketing na kukuuliza lugha
unayotaka kutumia.
“Ukishachagua lugha, utakuja ujumbe utakaokutaka ujaze kituo
unachotoka. Kama upo Dar, Mbeya au sehemu yoyote utajaza, kisha utapata
ujumbe unaokutaka ujaze unakokwenda, utapata ujumbe unaokuuliza kampuni
ya basi unayotaka kusafiri, tarehe ya kusafiri, utakuja ujumbe wa
kukutaka uchague nauli unayotaka kulipa.
“Baada ya hapo utachagua kiti unachotakiwa kukaa kama ni dirishani au
sehemu yoyote na kisha utapata maelezo ya tiketi yako,” alisema.
Kaswahili alisema ikifika asubuhi, abiria anapaswa kwenda na ujumbe wa
tiketi yake kwenye simu na kama ujumbe huo umefutika kwa bahati mbaya,
anatakiwa kutaja namba aliyotumia kununulia tiketi na kuonesha
kitambulisho.
Alisema changamoto waliyonayo kwa sasa ni ya uelewa kwa abiria na
wenye mabasi hivyo wanahitaji elimu zaidi juu ya huduma hiyo.
Alitoa wito kwa wateja na kuwataka abiria kujiandaa na mabadiliko hayo kwa ajili ya kuondoa usumbufu kwao.
No comments:
Post a Comment