Dar es Salaam.
Vilio, simanzi na maombi ya kunena kwa lugha vilitawala jana katika Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), Temeke Dar es Salaam wakati waumini na ndugu wa Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dk Moses Kulola (83) walipopata taarifa za kifo cha kiongozi huyo.
Vilio, simanzi na maombi ya kunena kwa lugha vilitawala jana katika Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), Temeke Dar es Salaam wakati waumini na ndugu wa Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dk Moses Kulola (83) walipopata taarifa za kifo cha kiongozi huyo.
Katibu Mkuu wa EAGT, Brown Mwakipesile alisema kuwa Askofu Kulola alifariki dunia jana saa tano asubuhi kwenye Hospitali ya Africa Medical Invesment (AMI), Dar es Salaam.
Mwakipesile alisema afya ya Askofu Kulola ilianza kubadilika Mei mwaka huu akiwa mkoani Mwanza ambako alipelekwa Hospitali ya Rufaa Bugando ambako alibainika kuwa na matatizo ya moyo.
“Kanisa liliamua kuchukua jukumu la kumpeleka Hospitali ya Apollo, India kwa matibabu zaidi na baada ya kuona afya yake inatengemaa aliruhusiwa kurejea nchini, lakini Agosti 16, mwaka huu hali ilibadilika ndipo tukampeleka AMI alikofikwa na mauti,” alisema Mwakipesile.
Alisema kifo hicho kimeacha pengo kubwa ambalo haliwezi kuzibwa kwa sasa. Hata hivyo, wanafarijika kwa upande mwingine wakiamini kwamba Mungu amemchukua mtumishi wake kwa wakati alioukusudia.
Alisema mwili wa Askofu Kulola utasafirishwa
kwenda Mwanza Jumamosi jioni kwa ndege baada ya kuagwa kanisani hapo.
Atazikwa kwenye Uwanja wa Kanisa la EAGT Bugando.
Askofu Kulola ni mmoja wa viongozi wa dini
waliokuwa na jina kubwa nchini na alifanya kazi za utumishi wa kanisa
kwa miaka 53 kwa kuhubiri na kuwaombea wenye matatizo mbalimbali.
Mtoto wa kwanza wa askofu huyo, Goodluck Kulola alisema wamejifunza mambo mengi katika maisha ya baba yao, ikiwamo upendo na unyenyekevu ulioongozwa na uchaji Mungu.
“Baba alikuwa ni asiyependa kabisa migogoro ya kidini, kisiasa yaani ikitokea hali ya uvunjifu wa amani wa namna yoyote ile alikuwa anaumia sana. Alipenda watu kwa ujumla ametufundisha upendo.”
Askofu Kulola ameacha mke wake aitwaye Elizabeth, ambaye alibarikiwa kupata naye watoto 10 na wengine wawili wa kuasili. Hata hivyo, watoto watatu walishafariki dunia. Ameacha wajukuu 44 na vitukuu 10.
Askofu Kulola, ambaye alizaliwa 1928, alianza Shule ya Misheni ya Ligsha Sukuma mwaka 1939, baadaye alijiunga na Shule ya Bwiru kabla ya kusomea Usanifu Majengo huko Israel kisha kuanza kazi ya kumtumikia Mungu mwaka 1950.
Alifuzu Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Theolojia katika Chuo Kikuu cha California State Christian Marekani.
Aliwahi kutumika kwenye Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) mwaka 1966 mpaka 1991 alipoamua kuanzisha Kanisa la EAGT lenye matawi katika nchi za Zambia, Malawi, Burundi na Msumbiji.
Rais Jakaya Kikwete jana alituma salamu za rambirambi kutonana na kifo cha Askofu Kulola
Aliwahi kutumika kwenye Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) mwaka 1966 mpaka 1991 alipoamua kuanzisha Kanisa la EAGT lenye matawi katika nchi za Zambia, Malawi, Burundi na Msumbiji.
No comments:
Post a Comment