Dodoma. Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji
Frederick Werema jana ameangukia pua baada ya Bunge kukataa mapendekezo
ya Serikali ya kubadili baadhi ya vipengele vya Sheria ya Magazeti ya
mwaka 1976, ya kuongeza adhabu kwa waandishi wa habari watakaopatikana
na hatia ya makosa ya uchochezi.
“Mheshimiwa Spika, nimesimama kuona hata wa upande wangu wamenisaliti, duh, basi naomba kura zihesabiwe kwa kuita majina mmoja, mmoja ili tujiridhishe,” alisema AG Werema jana.
Kadhalika Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliungana na wabunge wengine kukataa mapendekezo hayo na kudai kuwa wakati umefika kwa Serikali kupeleka bungeni muswada wa sheria ya vyombo vya habari, badala ya kutoa ahadi zisizo na majibu kila wakati.
Kukataliwa kwa mapendekezo hayo ni pigo kwa Serikali na Jaji Werema ambaye juzi wakati akijibu hoja za wabunge alijigamba kwamba yeye anasimamia amani ya nchi kwa hiyo vifungu hivyo haviwezi kuondolewa, kwani anafanya kazi kwa masilahi ya taifa na hategemei magazeti kwa ajili ya kuwa mbunge.
“Sitegemei magazeti kuwa mbunge nafanya kazi ya
taifa. Walio wangu watanikataa na wasiokuwa wangu watanikataa. Nipo kwa
ajili ya taifa sitamwangukia mtu yeyote miguuni,” alisema Werema, kauli
ambayo iliwachefua wabunge.
Hata hivyo, jana baada ya Spika kuwahoji wabunge na kukataa mapendekezo ya Serikali, Jaji Werema alionekana kukereka hivyo alisimama na kutaka Spika aruhusu kura zihesabiwe katika kifungu hicho.
“Mheshimiwa Spika, nimesimama kuona hata wa upande wangu wamenisaliti, duh, basi naomba kura zihesabiwe kwa kuita majina mmoja, mmoja ili tujiridhishe,” alisema Werema.
Hata hivyo, Spika alikataa na kusema: “Kama kuna
eneo ambalo tumefanyia utani Serikali ni katika eneo hili, naomba
Serikali mtuletee muswada bungeni siyo porojo za maneno.”
Katika marekebisho hayo, Serikali ilikuwa ikipendekeza katika sheria hiyo mabadiliko ya kuongeza adhabu kwa waandishi wa habari watakaopatikana na hatia ya kuandika habari za uchochezi, kutoka faini ya Sh15,000 hadi kiasi kisichozidi Sh5 milioni.
Hata hivyo, wakati Bunge lilipoketi kama kamati wabunge walikataa kupitisha marekebisho hayo ambayo yalikuwa sehemu ya Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa mwaka 2013, wakisisitiza kwamba Serikali ipeleke bungeni muswada wa sheria ya habari.
Moto wa wabunge
Moto wa wabunge hao uliwashwa na Mbunge wa Kigoma
Mjini, Peter Serukamba (CCM), ambaye alipendekeza sehemu ya nane ya
muswada iliyokuwa na vipengele vya 39, 40 na 41 iondolewe ili
kuishinikiza Serikali kupeleka bungeni sheria nzima inayohusu vyombo vya
habari.
Mbunge huyo alisema kuwa sehemu hiyo na vipengele
vyake kama vingepitishwa vingeifanya Serikali kuwa kimya na kushindwa
kupeleka bungeni Muswada wa Sheria ya Vyombo vya Habari kama ilivyoahidi
kwa muda mrefu.
No comments:
Post a Comment