KWA wasiomfahamu msichana huyu,
wanamuona kama chipukizi aliyeukwaa ustaa ghafla, lakini wanaofuatilia
mambo ya sanaa na burudani, wanamfahamu kitambo. Ninamzungumzia Snura
Mushi, ambaye anatamba sana na kibao chake cha Majanga.
Ni
mmoja kati ya wasanii wapambanaji, wakisaka mafanikio kwa kujaribu kila
aina ya njia. Amejaribu kwa muda mrefu katika filamu, lakini hakuweza
kufanikiwa ‘kuchomoka’. Kama angetambua tokea mapema kuwa angeweza
kuibuka mara moja katika muziki, nadhani asingepoteza muda wake mwingi
kwenye filamu.
Wimbo wake wa Majanga umeiteka familia ya muziki wa mduara, huenda
kwa sasa ni mmoja kati ya wasanii wachache wanaopata nafasi ya kutakiwa
sana katika majukwaa na hivyo kumfanya pia awe anapata hela za kutosha.
Katika
uigizaji, alifanikiwa kucheza vizuri katika filamu kadhaa, ingawa kama
ninavyosema mara zote, viwango vibovu vya sinema za Tanzania vilisaidia
kumfanya asing’ae!
Wimbo wa Majanga imempandisha sana chati, kwani licha ya maneno yake
yaliyopangiliwa vizuri, pia midundo yake imeongeza thamani ya kibao
hicho.
Lakini kama kuna kivutio zaidi katika maonyesho ya Snura, hasa
katika wimbo wake huu, basi ni yeye mwenyewe. Ni kivutio kwa sababu
anacheza wimbo wake kwa namna ambayo, ni mchanganyiko wa mshangao na
hamasa za kingono.
Licha ya kucheza kwa umahiri mkubwa huku akikitumia zaidi kiuno
chake, hali huwa tete pale anapoyatingisha na kuyatetemesha makalio yake
huku akiwa amewapa mgongo mashabiki wake ambao hulipuka kwa shangwe.
Uvaaji
na uchezaji wake hauvutii machoni mwa watu wenye kuzingatia maadili ya
Kitanzania, kwa maana ya tabia njema. Ni kweli anashangiliwa sana,
lakini natia shaka kidogo kama kinachoshangiliwa ni muziki wake au ni
namna anavyocheza.
Akili yangu inaamini anashangiliwa kwa namna anavyocheza. Na kama
hivi ndivyo, basi si jambo la kujivunia hata kidogo. Uchezaji wa msanii
huyu, haustahili mbele ya watoto wetu wanaoupenda muziki wake na wala
haupendezi machoni mwa wanaharakati wa maadili.
Binafsi ninaamini Snura ameshauwezea aina ya muziki wake huu, ndiyo
maana ameanza kupata washindani kama Shilole, ambaye naye kwa bahati
mbaya, anaamini katika kukata mauno, uvaaji usiofaa na ufundi wa
kuchezea viungo vyake!
Uchezaji na uvaaji wake unaonekana pia nchi
nzima kupitia video yake. Ni wazazi wachache wanaoweza kufurahia
kuutazama wakiwa na watoto wao.
Kuna wakati nilipata kumsikia akitangaza kusaka mtu wa kumuoa. Kwa
uchezaji ule jukwaani, sidhani kama anaweza kumpata mume anayemhitaji,
isipokuwa watu wengi wenye tamaa ya ngono wanaweza kujitokeza. Hakuna
mume makini anayeweza kukubali mkewe acheze na kuvaa namna ile.
Labda kwa faida yake binafsi nimshauri kujitazama upya kwa sababu
kubadilika ni sehemu ya maisha. Kama anafikiri uvaaji na uchezaji ule
ndiyo unampatia mashabiki, mimi nakataa kwa sababu najua muziki wake
umekubalika, anaweza kuvaa na kucheza kawaida na bado akaendelea kuwa
juu.
Ni vyema wasanii wetu wakatambua kwamba ustaa wao unawafanya
wawe mfano. Huenda zile shangwe zinazotoka kwa mashabiki siyo za kumsifu
kwa uhodari wake, bali ni kumzomea kwa jinsi anavyojidhalilisha.
Na pengine ni wakati muafaka pia kwa Baraza la Sanaa la Taifa
(BASATA) kuanza kutembelea kumbi na matamasha ili kuwabaini na kujua
namna gani wanaweza kushughulika na watu wa aina hii. Hatuwezi kujenga
taifa lenye maadili kama kila mtu ataachiwa kufanya anachotaka kwa
sababu tu ya ustaa wao.
Kama wameweza kupiga kelele hadi sasa waigizaji wa filamu wameanza
kuvaa nguo zinazokubalika, hata huku kwenye muziki wa kizazi kipya
inawezekana. BASATA inao uwezo wa kuzipiga marufuku video na nyimbo
zisizoendana na utamaduni wetu.
CHANZO NI GPL
No comments:
Post a Comment