Jaji
Mkuu wa Tanzania Mh. Othman Chande (Kulia) akitoa ufafanuzi kwa
waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini mwaka
2015. Maadhimisho hayo yanaongozwa na maudhui yasemayo “ Fursa ya kupata
haki: wajibu wa Serikali, Mahakama na wadau”. Kushoto ni Mh. Hussein
Kattanga, Mtendaji Mkuu wa Mahakama.
Msajili
Mkuu wa Mahakama, Ignas Kitus (kulia) akizungumza akifafanua jambo
wakati Jaji Mkuu wa Tanzania Mh. Othman Chande alipokutana na waandishi
wa habari kuzungumzia maadhimisho ya Siku ya Sheria leo jijini Dar es
salaam.
Waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo leo. Picha na Aron Msigwa -MAELEZO.
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
Rais Jakaya Kikwete anatarijiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha
maadhimisho ya Siku ya sheria nchini (Law Day) itakayofanyika Februari
4, 2015, katika viwanja vya mahakama vilivyopo mtaa wa Chimala jijini
Dar es salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, Jaji
Mkuu wa Tanzania Mh. Othman Chande amesema kuwa maadhimisho hayo kwa
mwaka huu yanaongozwa na maudhui yasemayo “ Fursa ya kupata haki:
wajibu wa Serikali, Mahakama na wadau”.
Amesema kwa mara ya kwanza maadhimisho hayo yataambatana na
maonesho ya Wiki ya Shera yatakayofanyika katika viwanja vya Mnazi
Mmoja kuanzia tarehe 30 Januari 2015 hadi tarehe 2 Februari
2015 .
Mh.Chande ameeleza kuwa maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini na
maonesho ya Wiki ya Sheria yanaashiria mwanzo wa shughuli za mahakama
kwa mwaka 2015 na kufafanua kuwa kipaumbele kitatolewa katika kupunguza
mrundikano wa mashauri ya muda mrefu yaliyoko mahakamani na
kushughulikia mashauri yenye mvuto mkubwa kijamii,miradi mikubwa,
uhujumu uchumi, madawa ya kulevya, Biashara ndani na nje ya nchi na
Rushwa.
Kuhusu maonesho hayo amesema yanalenga kutoa elimu kwa wadau wa
sheria na huduma za kisheria kwa wananchi kuhusu Ufunguaji na uendeshaji
wa mashauri mbalimbali hasa mirathi, Utatuzi wa migogoro kwa njia ya
suluhu, kueleza mfumo mpya wa ulipaji wa tozo za kimahakama kwa njia ya
benki, Kutoa msaada wa kisheria, kutolewa vyeti vya mawakili, kupokea
maoni na malalamiko kwa ajili ya kuyatafutia ufumbuzi.
Ameeleza kuwa wadau wakuu watakaoshiriki katika maonesho hayo ni
Mahakama, Tume ya Utumishi wa Mahakama, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, Chuo cha Uongozi wa
Mahakama- Lushoto, Taasisi ya Mafunzo ya Uansheria kwa vitendo Tanzania
na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
Wadau wengine ni Taasisi zinazotoa msaada wa kisheria, TAKUKURU,
Jeshi la Polisi, Magereza, Chama cha Mawakili Tanganyika na Tume ya
kurekebisha sheria.
Amesema pamoja na maonesho hayo kutakuwa na matembezi maalum ya
kuadhimisha Wiki ya Sheria tarehe 1 Februari 2015 yatakayoongozwa na
Rais mstaafu wa awamu ya pili Mh. Ali Hassan Mwinyi kuanzia Mahakama
Kisutu kupitia barabara za Serena-Ohio, Gymkana –Obama Road, Mahakama ya
Biashara, Barabara ya Kivukoni, Sokoine , Railway, Nkurumah, Lumumba na
Mkunguni hadi Mnazi Mmoja.
No comments:
Post a Comment