MJADALA mzito wa bajeti ya serikali iliyowasilishwa Alhamisi
wiki iliyopita, utaanza kuunguruma leo, huku kambi ya upinzani bungeni
ikitabiriwa kuibua hoja nzito pale itakapowasilisha hotuba ya bajeti
mbadala ya fedha.
Taarifa za kuaminika kutoka ndani ya kambi ya upinzani inayoundwa na
wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), zinasema kuwa
hotuba hiyo mbadala ya bajeti, itakayosomwa leo, itaibua mambo mazito
ambayo yanaweza kuwatibua upya hata wabunge wengine ambao wamekuwa
wakiitetea ile ya serikali.
Kwa mujibu wa habari hizo, bajeti ya kambi ya upinzani imeandaliwa na
jopo la wachumi na wataalamu ambao ni wanachama wa chama hicho, na
ripoti sahihi za wasomi waliobobea katika nyanja na sekta zote muhimu
zikiwemo za madini, kilimo, miundombinu, elimu, afya katika ngazi za
kitaifa na kimataifa.
Imedaiwa kuwa bajeti hiyo, itaibua ‘madudu’ mengi ambayo yamefanywa na
serikali, ikiwemo hoja za matumizi ya fedha ambazo zilitolewa kwa zaidi
ya miaka mitano katika miradi ambayo baadhi yake haijakamilika na
mingine haipo, lakini kila mwaka inatengewa fedha.
“Kuna miradi mikubwa ikiwemo ya uzalishaji umeme ambayo kwa miaka
mitatu mfululizo imetengewa kiasi kikubwa cha fedha, lakini
haijakamilika na mingine haijaanza kabisa.
“Kibaya zaidi, serikali mwaka huu nayo imeomba fedha bila kusema zile
zilizotengwa kwa miaka ya nyuma zimeenda wapi na kwa nini mradi
haujaanza,” alisema mmoja wa wabunge walioshiriki kuandaa bajeti hiyo.
Semina yaibua hasira
Wakati hali ikiwa hivyo, jana kundi la wabunge wanaounda Chama cha
Kupambana na Rushwa (APNAC) walicharuka na kuafikiana kuichachafya
hotuba ya bajeti bila kujali tofauti za kiitikadi, baada ya kuelezwa
namna serikali inavyopoteza fedha kizembe.
Hasira za wabunge hao ziliibuka wakati wa semina iliyoandaliwa na
Taasisi ya Policy Forum, baada ya kuelezwa kinaganaga jinsi serikali
inavyopoteza mamilioni ya fedha kutokana na misamaha isiyo na tija kwa
taifa, huku ikiongoza kwa kuomba mikopo nje ya nchi.
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) aliweka wazi
jinsi makampuni ya madini yanavyoongoza kwa kuliibia taifa, kiasi cha
kuifanya sekta hiyo ishindwe kuchangia kikamilifu pato la taifa.
Alisema inashangaza sana kuona kuwa kiwanda cha bia kama Serengeti na
kile cha sigara ni miongoni mwa walipa kodi wakubwa 15 wakati kampuni
kama Baricck ikiwa haimo.
Kafulila aliliambia Tanzania Daima kuwa, ikiwa CCM italazimisha
kupitisha bajeti hii kwa vitisho, itakuwa imejimaliza kwa sababu
Watanzania wa sasa si wale wa juzi.
“Sioni pa kukwepa, na kama kuna mbunge anataka kuendelea na ubunge
wake hata akiwa ndani ya CCM, akubali kufia wapiga kura wake. Najua
wengi wanaipinga na wengi wameniambia hivyo,” alisema.
Akichangia zaidi, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Kessy Mohamed (CCM)
mbali na kuonesha masikitiko yake kwa namna bajeti ilivyo, aliwataka
wabunge kuwa makini katika masuala muhimu ya nchi.
Kessy alisema serikali imewaacha watu wakizurura ovyo, na kujiingiza
katika biashara zisizozalisha, hivyo kusababisha kupanda kwa bidhaa
muhimu nchini.
Katika hatua inayoonesha kuwa serikali itakuwa katika wakati mgumu
bungeni kuanzia leo, Waziri kivuli wa
Fedha, Kabwe Zitto ameeleza wazi
msimamo wa CHADEMA, kuwa wanaipinga bajeti hiyo kutokana na ukweli kuwa
haimlengi Mtanzania wa kawaida bali imelenga kuwanufaisha wachache.
Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, alitoa msimamo huo
juzi wakati akiwahutubia wananchi wa Kata ya Kihesa mjini Iringa.
Alisema kuwa, umasikini wa watu unasababishwa na mfumuko wa bei za
vyakula, huku serikali ikishindwa kudhibiti hali hiyo inayoendelea
kuwaumiza.
“Mfumuko wa bei umefikia asilimia 18.7 ambacho ni kiwango kikubwa sana
kwa maisha ya Mtanzania ambaye anatumia asilimia nane kununua chakula
na kipato chake kinazidi kushuka siku hadi siku badala ya kupanda
kutokana na rasilimali zilizopo,” alisema Zitto.Alifafanua kuwa, mfumuko
wa bei za vyakula pekee umefikia asilimia 25 na ule wa bei ya nishati
ukiwa kwenye asilimi 28 huku deni la taifa likizidi kukua kila siku.
“Kama leo tukilazimika kulipa deni la taifa, basi kila mtu kuanzia
mtoto atakayezaliwa leo hadi wazee, atalipa sh 488,000,” alisema Zitto.
Habari na Charles Misango, Dodoma wa Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment