
Ujerumani yafuzu kwa robo fainali
Mashabiki wengi wanaifikiria timu ya Ujerumani imo katika nafasi nzuri ya kuwa bingwa Euro 2012
Lars Bender alifunga bao la
ushindi la Ujerumani siku ya Jumapili zikiwa zimesalia dakika 10 kabla
ya kipenga cha mwisho, na kuiwezesha nchi yake kuwa miongoni mwa nchi
nane ambazo zitashiriki katika michuano ya robo fainali.
Mechi nyingine ya kundi hilo la B ambayo
ilichezwa wakati mmoja, kati ya Ureno na Uholanzi, Ureno walifuzu kwa
ushindi kama huo wa magoli 2-1.
Bender,
mwenye umri wa miaka 23, na ambaye ni mchezaji wa Bayer Leverkusen ya
Ujerumani, aliizima ndoto ya Denmark ya mwaka 1992, walipowashinda
Wajerumani katika fainali.
Ujerumani iliweza kuongoza katika mechi hiyo
dakika ya 19 wakati Lukas Podolski alipofunga, lakini Michael
Krohn-Dehli aliweza kuisawazishia Denmark dakika sita baadaye na
kuipatia nchi yake matumaini ya kufika robo fainali.
Wachezaji wa Ujerumani hawakupendezwa na safari
kutoka kituo chao cha nyumbani cha Gdansk, Poland, hadi Ukraine, lakini
kutokana na ushindi wa Lviv, wameweza kufuzu kuingia robo fainali na
watafurahia kuicheza mji ambao wameezeka kambi yao.
Kabla ya mechi ya Jumapili, mara ya mwisho
Denmark ilipopambana na Ujerumani katika mashindano makubwa, ilikuwa ni
fainali ya 1992, wakati Yugoslavia ilipopigwa marufuku kucheza, na
hatimaye Denmark iliwashangaza wengi ilipoishinda Ujerumani katika
fainali.
Timu ya Ujerumani ya mwaka huu ndio timu yenye
vijana wenye umri mdogo zaidi katika mashindano ya mwaka huu, kwa jumla
wachezaji wengi wakiwa na umri wa miaka 25 na siku 107.
Hii ni mara ya kwanza kwa Ujerumani kukamilisha mechi za makundi kwa rekodi safi mno ya asilimia 100.
---------------------------------------------------------------------------------------------------------------
Ureno imo katika robo fainali

Cristiano Ronaldo aliiwezesha Ureno kuingia robo fainali
Mabao mawili ya mshambulizi
Cristiano Ronaldo yaliiwezesha Ureno kuingia robo fainali ya michuano ya
Euro 2012, kwa kuifunga Uholanzi, na pasipo shaka yoyote, kuwalazimisha
kurudi nyumbani.
Kwa Uholanzi kuwa na matumaini yoyote kuendelea
kusalia katika mashindano hayo, walilazimika kuifunga Ureno magoli 2-0,
na bao la kwanza la mkwaju wa kupinda kutoka kwa Rafael van der Vaart
liliwapa matumaini Uholanzi walipoweza kutangulia.
Lakini mchezo wa Uholanzi uliendelea kufifia, na Ronaldo alifanikiwa kusawazisha, alipopigiwa mpira na mwenzake Joao Pereira.
Nani alimsaidia Ronaldo kufunga kwa mara ya
pili, na Ureno ikavuka hatua ya makundi na kujiandikishia nafasi katika
robo fainali.
Ureno sasa itacheza na Jamhuri ya Czech, inayoongoza kundi A.
Kwa Uholanzi, timu hiyo imeonyesha mchezo duni
sana, kwa kushindwa katika mechi tatu za makundi, ilhali miaka miwili
iliyopita, wao walimaliza katika nafasi ya pili katika fainali ya Kombe
la Dunia nchini Afrika Kusini.
Itawachukua muda Uholanzi kumsahau Ronaldo,
mchezaji nyota wa Real Madrid ya Uhispania, ambaye aliifungia klabu hiyo
magoli 60 msimu uliopita, na katika mechi dhidi ya Jumapili alicheza
kwa kasi na kwa juhudi na kuwaacha Waholanzi wamezubaa.
No comments:
Post a Comment