Prof. Tibaijuka asema wabunge wanahitaji maombezi
WAKATI mjadala wa Bunge la Bajeti unaoendelea mjini Dodoma
ukitawaliwa na vijembe, kashfa, kejeli na maneno ya kuudhi, Mwenyekiti
wa Taasisi ya Kiislamu ya Imam Bukhary, Sheikh Khalifa Khamis Khalifa,
amesema mhimili huo wa dola umeoza na una udhaifu mkubwa unaotokana na
kiti cha Spika kukosa umakini na baadhi ya wabunge kukosa maadili wakati
wakijadili hoja zinazolihusu taifa.
Aidha sheikh huyo amelishambulia Bunge baada ya juzi kushindwa
kupitisha Bajeti ya Wizara ya Kilimo,
Chakula na Ushirika kutokana na
utoro uliosababisha kushindwa kufikia idadi ya wabunge wanaopaswa kuwamo
ukumbini wakati wa kupitisha bajeti kama kanuni inavyoelekeza.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Sheikh
Khalifa alisema mwenendo wa Bunge hivi sasa unahuzunisha kutokana na
tabia inayozidi kujengeka miongoni mwao ya kutumia uhuru wao vibaya.
Bila kutaja majina, sheikh huyo maarufu nchini alisema baadhi ya
wabunge na hata viongozi wa mhimili huo wanaenda kinyume na maadili ya
Kitanzania kwa kukosa staha na kutoa maneno ya dharau na kebehi hata
matusi kwa wabunge wenzao.
“Wabunge wetu wakati mwingine wanaonyesha kutojali heshima kwani
utashuhudia kijana mdogo anashindwa kuonyesha heshima kwa kiongozi wa
serikali au mtu mzima anayelingana na mzazi wake na wabunge au viongozi
wazee nao wanakosa staha kwa mbunge kijana na hivyo kulifanya Bunge
lionekane kama kijiwe cha wahuni,” alisema Khalifa.
Kwa mujibu wa Khalifa, vurugu ndani ya Bunge zinatokana na wabunge
wachache kutafuta umaarufu kwa njia ya mkato kwa kutotii kanuni za
Bunge na kwa kutumia lugha chafu.
“Wabunge wajue wananchi wanawaangalia. Binafsi naona malumbano hayo ni
jambo jema sana kwa sababu litawasaidia wananchi kuwa makini kuchagua
wabunge, hivyo mwaka 2015 tunategemea wananchi watasahihisha makosa
waliyofanya kuchagua baadhi ya wabunge ambao tabia zao zinakera na
hawafai kuendelea kubaki Bungeni,” alisema Khalifa.
Hivi karibuni wakati wa mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na
matumizi ya Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma) kwa mwaka wa
fedha 2012/2013 Mwenyekiti wa Bunge, Steven Mabumba, alishindwa
kuongoza kikao na kusababisha vijembe, kashfa, kejeli na maneno ya
kuudhi.
Mvutano na malumbano hayo ya kisiasa vilimfanya Mbumba kuonyesha wazi upendeleo kwa wabunge wa CCM dhidi ya wale wa upinzani.
Mabumba alifikia hatua ya kutoa hata kauli chafu Bungeni dhidi ya
Mbunge wa Ubungo (CHADEMA), John Mnyika, akisema mbunge huyo
“anawashwawashwa” na kutaka kusimama mara kwa mara kuomba mwongozo.
Baadaye alimtoa nje Mbunge Kasulu Moses Machali (NCCR Mageuzi) akidai
kuingilia mjadala huo na kuongeza kuwa alikuwa na ‘kiherehere’ cha
kudandia mambo yasiyomhusu.
Malumbano hayo yaliyoendelea kwa siku mbili, yalitokana na hoja ya
mgomo wa madaktari na jaribio la kutaka kuuawa kwa Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, ambaye alitekwa nyara katika
mazingira ambayo yanailazimisha serikali kuendelea kujitetea kwamba
haikuhusika kumteka daktari huyo.
Aliyeanza kuchafua hali ya hewa juzi Bungeni ni Mbunge wa Viti Maalum
na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya, ambaye alitoa tuhuma dhidi ya
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akisema kinahusika na
mgomo wa madaktari na kwamba waliomteka walivaa magwanda yanayoelekeana
na nguo wanazovaa wafuasi na wanachama wa CHADEMA.
Wakati Manyanya akiendelea kuzungumza, Mbunge wa Ubungo (CHADEMA),
John Mnyika, alisimama kupinga kauli hiyo na kumtaka msemaji athibitishe
au afute kauli yake.
Naye Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM) Mwigulu Nchemba aliungana na
Manyanya kwamba CHADEMA inahusika akitumia kauli kama za Manyanya.
Hoja hiyo ilimtibua Mnyika, akatumia kanuni mbalimbali kuwabana
wasemaji (Manyanya na Mwigulu), na kuwataka wathibitishe au wafute kauli
zao.
Hata hivyo kauli ya Manyanya imewasikitisha baadhi ya wabunge wa CCM kwa madai kuwa mkuu huyo wa mkoa wa Rukwa alipotoka.
Hadi sasa Mnyika aliomba mwongozo wa Spika kuhoji uhali wa Mwenyekiti
wa Bunge, Mabumba, kutumia lugha ya kuudhi kwa wabunge hao, lakini hadi
sasa kiti cha Spika hakijatolea uamuzi.
Malumbano mengine yaliibuka wiki iliyopita baada ya baadhi ya wabunge
kutaka kujadili chanzo cha ajali ya meli ya MV. Skagit iliyosababisha
vifo vya watu zaidi ya 150.
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), na Mbunge wa
Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), walitaka Bunge kujadili ajali ya meli
hiyo kama dharura.
Mambo yalianza kwenda kombo baada ya Lissu kuomba mwongozo wa Spika
kwa kutumia kifungu cha 47 (1) kikiambatana na kifungu cha 47 (3) cha
kutaka Bunge liahirishe shughuli zake na kujadili jambo la dharura la
taifa.
Katika mwongozo wake, Lissu alisema katika kipindi cha maswali
kulijitokeza swali linalohusu ajali za baharini, ambapo wabunge wengi
walionyesha hisia zao hasa kutokana na ajali ya meli ya Mv Skagit
iliyotokea juzi na kuua Watanzania wengi.
“Mheshimiwa Naibu Spika huu ni muda muafaka wa kulijadili suala hili
hasa ikizingatiwa kuwa ni muda mfupi tu tangu itokee ajali ya Spice
Islander na kuua idadi kubwa ya Watanzania inatokea tena ajali ya meli
kuzama na kupoteza maisha ya ndugu zetu, tujadili jambo hili kama
dharura,” alisema.
Baada ya kauli ya Lissu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisimama na kuliomba Bunge
lisijadili jambo hilo kwa kuwa hivi sasa taifa linashughulikia na
uokoaji pamoja na kuhifadhi miili ya marehemu.
Baadaye alisimama mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), akasema
ipo haja kwa jambo hilo kujadiliwa bungeni kama suala la dharura.
Alisema kuwa katika ajali nyingi zilizotokea za meli ikiwemo ya Mv
Bukoba na Mv Spice Islander kuliundwa tume kuchunguza ajali hizo lakini
matokeo yake hayakutolewa.
Mbunge wa Kasulu Mjini Moses Machali (NCCR-Mageuzi), aliomba mwongozo
na kuishutumu serikali kuwa imezoea kutoa hoja kuwa jambo fulani
linashughulikiwa na kusisitiza umuhimu ajali hiyo kujadiliwa bungeni
hapo kama dharura.
Akitoa mwongozo dhidi ya hoja ya Lissu, Naibu Spika wa Bunge Job
Ndugai, aliikataa hoja ya Lissu kwa madai hoja yake haikuungwa mkono na
wabunge licha ya kuitumia vizuri kanuni.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema, aliingilia kati
mabishano hayo na kufafanua kanuni hiyo kuwa inazungumza wazi kwamba
baada ya maswali mbunge ataomba mwongozo na kutoa hoja ya Bunge
kuahirishwa ili kujadili jambo la dharura kwa taifa.
“Waheshimiwa wabunge kwa hili Lissu alishatoa hoja, sisi binadamu tuna
vichwa tuvitumie kufikiri na si kufugia nywele tu,” alisema Werema
jambo lililoibua tafrani ambapo Lissu alidai ametukanwa na kutaka
mwanasheria huyo afute kauli yake,”
Lissu na baadhi ya wabunge wa chama hicho waliondoka bungeni humo kwa hasira.
Ndugai naye wakati fulani aliwahi kumkejeli Mbunge wa Kawe, Halima
Mdee (CHADEMA), kwamba wananchi wa jimbo hilo wamechagua kituko.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Profesa Anna Tibaijuka amewataka Watanzania kuwaombea viongozi wa ngazi
zote wakiwemo wabunge ili wapate hekima na busara kutoka kwa Mungu.
Akizungumza jana kwenye viwanja vya Jagwani wakati wa maombi maalum
kwa ajili ya taifa yaliyoandaliwa na Chama cha Kitume cha Karismatiki
Jimbo Kuu jijini Dar es Salaam Tibaijuka alisema kuwa wabunge wanapaswa
kisikilizana na kushindana kwa nguvu ya hoja na si vinginevyo.
Tibaijuka pia aliwataka waumini hao kuwaombea viongozi wa serikalini
nao ili wapate hekima sawa na aliyokuwa nao Baba wa Taifa Mwalimu
Julius Nyerere.
“Waumini wa Karismatiki naomba tuliombee Bunge, taifa na viongozi kwa
ujumla kwani wakifuata nyayo za Baba wa Taifa hakutakuwa na ufisadi wala
migomo na mtu anayezungumzia udini, itikadi za vyama au kubaguana huyo
ana matatizo ya akili,” alisema waziri huyo ambaye ni Mbunge wa Muleba
Kusini.
Mratibu wa Uinjilishaji Karismatiki Arbogasti Kanuti alisema wanafanya
maombezi ya mara kwa mara kwa kuwa dini hutengeneza watu wenye maadili
lakini wameamua kuliombea taifa kwa sababu sasa linapitia changamoto
nyingi ikiwemo rushwa, mauaji, migomo na upatikanaji wa Katiba mpya.
Via Asha Bani na Happiness Mnale wa Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment