AGIZO la Rais Jakaya Kikwete kuwataka madaktari wanaoendelea na
mgomo kuacha kazi limechukua sura mpya baada ya madaktari bingwa ambao
awali hawakuhusika kabisa na mgomo huo, kutoa tamko wakimtaka kiongozi
huyo wa nchi kuwatimua wao kwanza kabla ya wale wa ngazi ya chini.
Badala yake, madaktari bingwa ambao walitangaza kujiunga na wenzao
juzi, baada ya kupigwa na kujeruhiwa vibaya kwa Dk. Steven Ulimboka,
walisema wataendelea na mgomo wao hadi hapo serikali itakapowarejesha
kazini madaktari na madaktari wanafunzi wote waliofukuzwa.
Akitoa tamko la madaktari bingwa waliokutana kwa dharura jana na
kamati ya jumuiya ya madaktari kujadili hotuba ya rais Kikwete, kiongozi
wa mabingwa hao Dk. Catherine Mng’ong’o alisema huo ni msimamo wa
madaktari wenzake, huku akitaka kufunguliwa kwa meza ya majadiliano ya
dhati yenye nia ya kumaliza mgogoro wao.
“Madaktari bingwa hatuwezi kufanya kazi bila madaktari wa chini yetu…
kama serikali imedhamiria kuwafukuza kazi hawa na interns (waliopo
kwenye mafunzo ya vitendo) ianze na sisi.
“Tuko tayari kufukuzwa iwapo madai yetu ya msingi hayatatekelezwa na
kama kuondoka waanze kutufukuza sisi kwanza,” alisema Dk. Mng’ong’o
baada ya kumalizika kwa kikao cha madaktari bingwa kilichoketi kwa zaidi
ya saa tano kwenye viunga vya hospitali hiyo.
Alisema hata wao hawana sababu ya kuendelea kufanya kazi katika
mazingira magumu na kuwaona Watanzania wakifa kwa kukosa vifaatiba na
dawa.
Dk. Mng’ong’o alisema madaktari hapa nchini wamefanya kazi katika
mazingira magumu kwa muda mrefu hivyo wakati wa kubadili hali hiyo
umefika na kuwasaidia Watanzania maskini wanaotibiwa kwenye hospitali
hizo.
Jumuiya yasema JK kadanganywa
Kwa upande wao viongozi wa Jumuiya ya Madaktari nchini wameelezea
masikitiko yao, ya namna Rais Kikwete alivyopewa taarifa za uongo na
wasaidizi wake.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya jengo la watoto kwenye
hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Katibu wa Jumuiya hiyo Dk. Edwin
Chitage alisema wako tayari kumweleza ukweli rais kwa kuwa wasaidizi
wake wameshindwa kufanya hivyo.
“Rais hajapata taarifa sahihi… tuko tayari kumweleza ukweli kwa sababu
wasaidizi wake wanamdanganya, tunasikitika kuona watanzania
wakidanganywa.
“Wanaelezwa hoja dhaifu za kuonyesha kwamba madaktari hatuna uzalendo
wakati madai yetu pia ni kwa maslahi ya wagonjwa wote hasa pale
tunapodai mazingira bora ya kazi.
Katibu huyo alisema moja ya madai yao yalikuwa kuomba kila hospitali
ya wilaya ipate mashine moja ya X-ray kwa vile, haiwezekani nchi nzima
kukosa mashine ya CT-Scan wakati bei yake ni sawa na gari aina ya
shangingi moja la kiongozi wa serikali,” alisema Dk. Chitage.
Katibu huyo alikiri kwamba posho ni sehemu ya madai yao huku
akisisitiza kwamba hawang’ang’anii nyongeza hiyo badala yake kuwepo
kwanza na mazingira bora ya kazi ili kutoa tiba sahihi kwa mgonjwa.
Dk. Chitage alisema hawapendi kubishana na mamlaka ya rais huku
akisisitiza uwezo wa kumaliza hili ni Kikwete kukaa nao meza moja kwa
ajili ya kuzungumza badala ya kutoa vitisho.
Waomba kukutana na Rais
Madaktari hao walisema kuwa sasa wanaomba kukutana na rais ili kujadili hatima ya mgomo huo.
“Tunamheshimu rais na mamlaka zote ila tunachoamini ni kuwepo kwa meza
huru ya majadiliano kati yetu na yeye kwa sababu nafasi ya kumaliza
kero hii anayo,” alisema.
Naye Makamu Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Dk. Godbless Charles alihoji
sababu za kuwepo kwa taarifa tofauti kuhusu ongezeko la mishahara wakati
waliishauri serikali kuwa wazi kuhusu nyongeza hiyo.
“Kumekua na majibu tofauti mfano Waziri wa Afya na UStawi wa Jamii
aliliambia Bunge kwamba nyongeza ya mishahara ni asilimia 15. Hotuba ya
rais Kikwete inasema nyongeza hiyo ni asilimia 20 wakati ripoti ya
wataalam iliyokutana na kamati ya Waziri Mkuu ilipendekeza asilimia 25
je, nia ya serikali iko wapi?
“Wakati viongozi wa serikali wakitoa taarifa zinazotofautiana ripoti
ya ufafanuzi wa madai na hoja za madaktari iliyotokana na majadiliano
ambapo tulikuwa wajumbe hatukutoa pendekezo lolote juu ya ongezeko la
mshahara,” alisema Dk. Godbless.
Alisema tangu kuanza kwa mgogoro kati ya madaktari na serikali jumla
ya vikao sita viliketi kati ya hivyo vikao vinne vilijadili juu ya
uboreshaji wa huduma za afya kwa watanzania.
“Ni masikitiko yetu kuwa ripoti ya ufafanuzi wa hoja na madai yetu
iliyotolewa Juni 31 mwaka huu, taarifa ya waziri wa afya, taarifa ya
waziri mkuu ndani ya Bunge na hotuba ya rais haikuzungumzia kwa jinsi
gani serikali itaboresha huduma za afya kwa watanzania,” alisisitiza Dk.
Godbless.
Katika hotuba yake kwa wananchi rais Kikwete aliwataka madaktari wote
waliogoma kuchakazi kwa kuwa viwango vikubwa vya mishahara wanaoitaka
serikali haiwezi kuilipa.
Kipigo cha Dk. Ulimboka
Akizungumzia kutekwa, kupigwa na kutelekezwa kwenye msitu wa Pande
alikofanyiwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania Dk. Steven
Ulimboka alisema wameshtushwa na kauli ya rais Kikwete.
Kwa mujibu wa Dk. Godbless kauli ya rais Kikwete kwamba serikali yake
haihusiki na kitendo hicho kimeingilia uhuru wa tume hiyo ambayo tangu
awali madaktari na wanaharakati waliipinga.
“Tume imeundwa kuchunguza suala hilo na mpaka sasa hakuna mwenye uwezo
wa kudhibitisha kwamba serikali inahusika… je ni sahihi kwa rais
kutangaza waziwazi kwamba serikali yake haihusiki?
“Kauli hiyo haitoi uhuru kwa tume kueleza ukweli wa tukio kwa sababu
tume hiyo imeundwa na serikali yenyewe,” alisema makamu mwenyekiti huyo
na kuongeza kwamba madaktari hawana imani na tume hiyo.
Awali alisema madaktari wana hasira kwa kitendo cha kinyama
alichofanyiwa mwenzao hali inayowafanya waishi kwa hofu huku wengine
wakiandika barua za kuacha kazi na wengine wakiendeleza mgomo.
Bunge lachafuka, kupigwa Ulimboka
Katika hatua isiyokuwa ya kawaida, hali ndani ya bunge jana jioni
ilichafuka, baada ya mwenyekiti wa bunge, kushishwa kabisa kuongoza
kikao hicho kufuatia kuzuka kwa malumbano makali baada ya Mkuu wa mkoa
wa Iringa, Stella Manyanya kukituhumu Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) kuwa vinara wa mgomo wa madaktari.
Manyanya alisema kuwa, CHADEMA wamebainika kuchochea mgogoro huo, hali
iliyomfanya Mbunge wa Ubungo kusimama na kuomba mwongozo akimtaka
Manyanya kuthibitisha ama kukanusha tuhuma hizo.
Lakini katika hali ya kushangaza, Mbunge wa Iramba mashariki Mwigulu
Mchemba alisimama na kunukuu hotuba ya kambi ya upinzani, ambayo
ilitamka bayana kuwa inaunga mkono madai ya watumishi wa serikali, na
kwamba kwa kauli hiyo inadhihirisha bayana kuwa ndio wakuu wa mgomo huo.
Badala ya kutoa mwongozo, Mabumba hakumtaka Manyanya kukanusha ama
kuthibitisha alimruhusu
Mchemba kuendelea kurusha makombora mazito dhidi
ya CHADEMA, safari hii akidai kuwa ni vimbelembele kutoa matamshi ya
kulaani kupigwa kwa Ulimboka huku, wakimwacha mmoja wa viongozi wake
bila kumhudumia wala kumjulia hali.
Katika kujichanganya kwa wabunge hao wa CCM, wakati Mchemba akidai
kuwa CHADEMA ndio wachocheaji wakubwa wa mgogoro huo kwa kuwatumia
madaktari, mwenzake Manyanya alitoa hoja safari hii akidai kuwa, ndio
waliohusika na tukio la kumvamia na kumteka na kisha kumpiga Dk.
Ulimboka.
Hata pale Mnyika aliposimama na kuomba tena mwongozo wa mwenyekiti,
huku akiweka bayana jinsi inavyoelezwa ushiriki wa maafisa wa polisi, na
hata Dk. Ulimboka mwenyewe kuwataja wengine kwa majina, alimtaka
mchangiaji kuthibitisha ushiriki wa CHADEMA kumjeruhi ama siyo afute
kauli yake.
Lakini kwa mara nyingine tena, Mabumba hakumtaka Manyanya wala Mchemba
kuthibitisha kauli ama kufuta kama inavyofanywa kwa wabunge wa
upinzani, badala yake alimruhusu mkuu huyo wa mkoa wa Iringa kuendelea
na mchango wake bila kufuta kauli wala kuithibitisha.
Kushindwa huko kwa waziwazi kwa Mwwenyekiti wa kikao hicho cha bunge,
kuliwachefua wabunge wengi wa upinzani, huku wale wa CCM wakionekana
kufurahia jambo hilo.
Via Tanzania Daima 3/7/2012
No comments:
Post a Comment