MTOTO wa ajabu amezaliwa katika Hospitali ya Mkoa wa Singida
huku akiwa hana baadhi ya sehemu za mwili wake kuanzia kifuani hadi
kichwani.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Singida, Dk. Joseph
Malunda amesema tukio hilo ni la mara ya kwanza katika Hospitali hiyo.
Kwa mujibu wa daktari huyo mama wa mtoto huyo alikuwa amejifungua
watoto wawili pacha wote wa kike wakiwa na miezi saba huku mmoja akiwa
na viungo vyote.
Dk.Malunda alidai mama wa watoto hao Amina Bilau baada ya kujifungua
mtoto wa kwanza, alifuatia mtoto mwingine ambaye hakuwa na mikono, kifua
na kichwa.
Hata hivyo, mtoto wa kwanza aliweza kuishi kwa saa sita tu na kufariki.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Malunda alitumia fursa hiyo kuwashauri
akina mama wanapopata ujauzito wasisite kuhudhuria kliniki na kuacha
kutumia madawa makali yanayoweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kuzaliwa
watoto wenye upungufu wa viungo.
Akizungumzia tukio hilo, Amina Bilau mkazi wa Kijiji cha Mtamaa katika
Halmashauri ya Manispaa ya Singida alisema wakati wa ujauzito wake yeye
aliona tumbo lake likiongezeka, na baada ya kupata matibabu katika
zahanati ya Kijiji bila mafanikio na akaamua kwenda katika Hospitali ya
Mkoa wa Singida na kisha kujifungua watoto hao.
Baba wa watoto hao, Maulidi Mkuki alisema hata yeye anashangaa kuona
mkewe amejifungua mtoto wa aina hiyo wakati wana watoto wengine watatu
waliozaliwa bila matatizo yoyote yale.
‘’Kwa kweli naona ni ajabu kwa mama kujifungua mtoto na ‘mdoli’ alisema Mkuki akiwa na masikitiko.
Habari na Jumbe Ismailly, Singida
No comments:
Post a Comment