WIZARA Elimu na Mafunzo ya Ufundi imesema inajiandaa kupeleka
bungeni vigezo vipya vya kukopesha wanafunzi wa elimu ya juu ambavyo
vinatarajiwa kuanza kutumika mwaka huu wa fedha.
Hayo yalielezwa jana mjini hapa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi Philipo Mulugo Wakati akijibu swali la mbunge wa Chwaka Yahya
Kassim Issa (CCM) aliyetaka kujua suala la upatikanaji wa mikopo namna
linavyokwenda kwa kuwa linaonekana kutolewa kwa ubaguzi na kujuana.
Akijibu swali hilo Mulugo alisema tayari wizara yake ilishavifanyia
mabadiliko vigezo hivyo na tayari ilishaviwasilisha kwenye Kamati ya
Maendeleo ya Jamii chini ya uongozi wa mwenyekiti wake Margareth Sitta.
Alisema suala hilo halina upendeleo hata kidogo na kwamba vigezo
vinavyotumika vipo wazi kwa kila mtu na tayari vimeshafanyiwa mabadiliko
kama walivyoagiza waheshimiwa wabunge.
Katika swali la msingi mbunge wa Baraza la Wawakilishi Jaku Hashimu
Ayoub alitaka kujua ni vigezo gani muhimu vimetumika kujenga vyuo vikuu
vyote vya taifa upande mmoja wa Muungano wakati elimu ndio msingi mkuu
wa maendeleo ya wananchi wake.
Mulugo alisema vyuo vikuu havianzishwi kwa maana ya kuongeza idadi
bali kwa madhumuni maalum kutegemea mahitaji halisi, uwezo wa kifedha wa
serikali lakini kwa kiasi kikubwa unategemea sekta binafsi ambayo
imetoa mchango mkubwa katika ukuzaji wa elimu ya juu pande zote za
Muungano.
Aidha alisema uanzishwaji wa vyuo unategemea uwepo wa wadau wakiwemo
wanafunzi wenye sifa, rasilimali watu, mtaji, wahadhiri, miundombinu na
vifaa vya kufundishia na kujifunza pamoja na madhumuni halisi ya
kuanzisha Chuo Kikuu husika.
Na Happiness Mtweve, Dodoma
No comments:
Post a Comment