WAKATI walimu wamesitisha mgomo wao, Chama Cha Walimu (CWT)
kimetilia shaka hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi
kwamba ina mkono wa Rais Jakaya Kikwete.
CWT imesema inatilia shaka hukumu hiyo kwa madai kuwa maneno
aliyoyatumia Jaji Sophia Wambura kusoma hukumu iliyobatilisha mgomo wa
walimu, inafanana na kauli ya Rais Kikwete aliyoitoa siku moja kabla,
wakati wa mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari uliofanyika
Ikulu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Rais wa
CWT, Gratian Mukoba, alisisitiza kuwa Rais Kikwete aliingilia kati
hukumu hiyo kwani katika mazingira ya kawaida, kauli yake isingepaswa
kufanana na ya Jaji Wambura.
“Rais Kikwete alichokiongea ndicho ambacho kimetolewa na kutekelezwa
na Jaji Wambura. Inaonyesha wazi kwamba kulikuwa na mawasiliano kati
yake na jaji ili kutimiza malengo ya serikali,” alisema.
Hata hivyo, Mukoba alisema kuwa wanatii hukumu hiyo na kuwaagiza
walimu wote nchini kurudi kazini kuanzia jana ili kutekeleza majukumu
yao, na maagizo mengine yatatolewa baada ya kuipitia hukumu.
Kuhusu kulipa fidia ya hasara ambayo serikali inadai kuipata kutokana
na mgomo huo, Mukoba alisema chama chake kinasubiri taarifa rasmi ya
serikali kwani hakina uwezo wa kufahamu hasara iliyotokana na mgomo wao.
Mukoba alisema chama hicho kitaendelea kupigania madai ya walimu na
kuhakikisha serikali inayatekeleza kwa kuwa hata hukumu iliyotolewa
haikupingana na madai yao.
Rais huyo ambaye ni mwalimu wa Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa ya
jijini Dar es Salaam, alisema anashangazwa na taarifa ya Rais Kikwete
kudai kuwa madai ya walimu hayatekelezeki wakati fedha hizo za mishahara
zikigawanywa kwa usawa kila mtumishi atapata kwa haki.
Alisema kuwa hukumu hiyo imewakatisha tamaa walimu pamoja na kurudi
kazini, huku ikionesha dhahiri kuwa serikali haiwajali kutokana na madai
yao kutopewa kipaumbele.
Akinukuu maneno ya hayati Mwalimu Julius Nyerere, Mukoba, alisema:
“Mwalimu alisema kuwa mganga wa kienyeji mara zote huvaa ngozi ya simba
ili kuwatisha wagonjwa, hivyo hata serikali inatangaza madai ya walimu
hayalipiki ili Watanzania wakubaliane nao.
“Hata siku moja mgomo halali hauwezi kutokea hapa nchini kwa kuwa
sheria zinapindishwa, lakini nchi nyingine sheria hizi ndizo
zinazotumika, na hata hivyo wenzetu wapo wazi na kujua kile serikali zao
zinachoingiza kuliko ilivyo hapa kwetu,” alisema.
Rais huyo, alisema kwa takwimu za GDP (kiwango cha ukuaji uchumi)
zilizopo zinaonesha kuwa ni asilimia 41 tu inatumika kwa ajili ya
mishahara wakati asilimia 59 zinatumika kulipana posho, hivyo alishauri
kuwa kama serikali ni sikivu, ipunguze viwango vya posho.
“Siku zote ukitaka kumchinja kobe lazima umvizie, ukimjumlisha lazima
atarudisha shingo yake ndani, hivyo serikali inapotaka ipewe taarifa za
mgomo mapema ni sawa na kuwaambia wajiandae kuukabili,” alisema.
“Ukiona watoto ndani ya nyumba wanapiga kelele basi ujue hakuna amani
na wakifikia hatua ya kupiga kelele nje ujue kuwa wamemchoka mzazi wao.
Ndivyo ilivyo kwa walimu,” alisisitiza.
Kuhusu kuwapo kwa taarifa za baadhi ya walimu kutoa mafundisho ya
masomo kwa kupotosha kwa makusudi, alisema CWT haina uwezo wa kulizuia
hilo, na kama serikali inataka kudhibiti tabia hiyo ni bora iharakishe
mazungumzo yake na walimu.
Akizungumzia suala la ulinzi na usalama wao, Mukoba alisema CWT ina
wasiwasi na viongozi wao walioitisha mgomo na kuitaka serikali
kuwahakikishia usalama wao yasije yakawakuta yaliyomtokea kiongozi wa
Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka aliyetekwa, kupigwa na
kujeruhiwa na watu wasiojulikana.
“Nashukuru Mungu sijapelekwa kule ambako Dk. Ulimboka alifikishwa,” alisema Mukoba huku akicheka.
Julai 29, mwaka huu CWT ilitangaza mgomo wa walimu nchi nzima hatua
ambayo ilipingwa na serikali na baadaye ilikimbilia mahakamani kuuzuia.
Juzi, Jaji Wambura alisema mgomo huo ni batili kwani haukuzingatia
matakwa ya kifungu cha 84(1), (2) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazi
ya mwaka 2004.
Kutokana na uamuzi huo, Jaji Wambura alimtaka mdaiwa (Chama cha Walimu
Tanzania - CWT) aliyetangaza mgomo huo kutumia vyombo vya habari
kueleza kuwa mgomo huo ni batili pamoja na kuwataka walimu kurejea
kazini mara moja.
Katika hatua nyingine, hukumu hiyo imepingwa vikali na wananchi,
viongozi wa vyama vya wafanyakazi pamoja na vyama vya siasa mkoani
Mwanza, na kusema mahakama hiyo haijawatendea haki walimu.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi jana kwa nyakati tofauti,
viongozi na wananchi hao walieleza kusikitishwa na amri hiyo ya mahakama
dhidi ya madai ya walimu, na kwamba hukumu za namna hiyo zinaweza
kuvuruga amani ya taifa.
Walisema, hawaoni sababu ya mahakama hiyo kuzuia mgomo huo wa walimu
wa kushinikiza kulipwa nyongeza ya mishahara na posho zao, hivyo wao
wanaona hali hiyo imelenga taifa kuendeleza matabaka ya watumishi
wanaolipwa mishahara minono na wanaolipwa kwa kiwango cha chini.
Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) Mkoa wa Mwanza,
Ramadhani Mwendwa na Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), mkoani hapa, Wilson Mushumbusi kwa ujumla wao waliipuuza
hukumu hiyo, kwa madai kuwa imeeegemea upande wa serikali.
Habari na Betty Kangonga
No comments:
Post a Comment