MKURUGENZI T-Moto Modern Taarab, Amin Salmin na Mkurugenzi wa Jahazi Modern Taarab, Mzee Yussuf, Jumamosi usiku almanusura wazichape kufuatia kutibuana kwao kwenye tamasha la Mitikisiko ya Pwani lililofanyika katika ukumbi wa Dar Live Mbagala.
Chanzo cha habari na www.saluti5.com
Wakurugenzi hao ambao daima tabasamu huwa haziwabanduki usoni walitibuana vibaya kiasi cha kutupiana matusi ya nguoni huku kila mmoja akitaka kumshikisha adabu mwenzake.
Mtafaruku wao ulianzia jukwaani wakati Jahazi wakitumbuiza wimbo wao wa pili kitendo kilichomfanya Amin Salmin apande jukwaani na kuwalazimisha waandaji wa tamasha hilo waishushe Jahazi jukwaani kwa vile utaratibu ulikuwa ni kila bendi kupiga wimbo mmoja na si nyimbo mbili.
Baada ya mvutano mkubwa hatimaye ikaamuliwa Jahazi wamalizie wimbo wao wa pili hali ilizozua manung’uniko mengi kutoka kwa Amin Salmin pamoja na baadhi ya viongozi wa bendi zingine.
Muda mfupi baada ya Jahazi kumaliza zamu yao ndipo mtafaruku mkubwa kati ya Amin na Mzee ulipoibuka jirani na geti la kutokea ambapo wawili hao walitupiana matusi huku kila mmoja akikunja shati kujiandaa na kichapo.
Watu walikuwa jirani pamoja na walinzi wa ukumbi huo walifanya juhudi kubwa kuwazuia wakurugenzi hao wasifikie hatua ya kutupiana makonde.
Amin alimwambia Mzee: “Usifikiri wote tuna vichwa vya nyanya, wengine tuna vichwa vya mapera chunga sana” Mzee Yussuf nae akamwambia kama wewe una kichwa cha pera si tuna vichwa vya nazi.
Amin Salmin aliimbia Saluti5 kuwa Jahazi wamekuwa wakibebwa katika kila idara kuanzia redioni hadi jukwaani. “Kila bendi iliambiwa ipige wimbo mmoja, T-Moto tukatii hilo bila ya kuongeza hata dakika moja katika muda tuliopangiwa, kwanini Jahazi wacheze rafu? Alihoji mtoto huyo wa Rais mstaafu wa Zanzibar Dr Salmin Amour.
Nae Mzee Yussuf katika maongezi yake na Saluti5 alisema wao hawakucheza rafu bali walilazimika kupiga wimbo wa pili baada ya kushauriana na waandaji kufuatia kelele nyingi za mashafiki waliofurika ukumbini hapo kuwataka wasishuke jukwaani.
“Tulizingatia zaidi suala la usalama tulihofia pengine mashabiki wangeweza kufanya fujo, ilibidi tuchukue uamuzi mgumu wa kutii amri ya mashabiki” alisema Mzee Yussuf na kuongeza kuwa wao kupiga nyimbo moja au mbili kusingewapunguzia au kuwaongezea chochote katika malipo yao hivyo hawakuwa na haja yoyote ya kukiuka ratiba iliyopangwa.
Haijulikani ni nini kitatokea pindi wawili hao watakapokutana mitaani kwani hata baada ya kuamuliwa ugomvi wao bado waliendelea kupeana ahadi ya kufundishana adabu popote pale watakapokutana.
No comments:
Post a Comment