Winga Mrisho Ngassa Juzi alipaswa kufanyiwa vipimo vya afya jijini Dar es Salaam chini ya viongozi wa timu hiyo ya Sudan, lakini katika hali ya kushangaza hakutokea. Alipohojiwa na vyombo mbalimbali vya habari, Ngassa alisema hayuko tayari kujiunga na El Merreikh kwa vile siyo Simba wala Azam iliyomshirikisha katika zoezi hilo.

Hata hivyo kauli ya Ngassa inapingana na aliyoitoa wakati akiwa na kikosi cha Timu ya Taifa Bara (Kilimanjaro Stars), akiitaka Simba iache kumbania kuchezea timu hiyo ya Sudan.
Makamu Mwenyekiti wa Simba Godfrey Nyange alisema wamesikitishwa na kitendo alichofanya Ngassa na kwamba watamwita ili kumhoji.“Hatufahamu nini kimempata mpaka sasa. Kwanza hao viongozi wa El Merreikh yeye binafsi ndiye aliyeongea nao na kufikia makubaliano,” alisema Nyange.

Nyange alisema wameshangazwa na uamuzi wa Ngassa wa kubadilika ghafla. “Pengine kuna kitu hapa, amebadilika ghafla,” aliongeza Nyange aliyeteuliwa kuzungumzia suala hilo pia kwa niaba ya Azam.
Simba na Azam zilitangaza kukubaliana kumuuza Ngassa kwa ada ya Dola 100,000 (Sh157 milioni). Katika makubaliano ya mkataba wa mchezaji huyo, El Merreikh ilidaiwa kuwa tayari kumpa Ngassa mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya Dola 75,000 (Sh118 milioni).