KOCHA Mkuu wa Timu ya Taifa ya soka Tanzania, ‘Taifa Stars’,
Mdenish Kim Poulsen, ameanika kikosi cha nyota 22 watakaoingia kambini
Januari 6, jijini Dar es Salaam kwa mechi za kirafiki akiwajumuisha
nyota wa kimataifa wataokipiga TP Mazembe ya DRC,
Mbwana Samata na
Thomas Ulimwengu.
Wakati Stars ikijiandaa na mechi ya kirafiki ya kimataifa
dhidi ya Zambia, Kim aliwaita wachezaji hao ambao licha ya kuripoti kambini, walishindwa kucheza kwa kuwa majeruhi.
Hiyo ni baada ya nyota hao kuwaliwasili nchini wakiwa na vyeti
vinavyoonesha kuwa ni wagonjwa, hivyo kuishia kukaa jukwaani
kuwashuhudia wenzao katika mechi hiyo ambayo Tanzania ilishinda bao 1-0
kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Kitendo hicho kiliibua sintofahamu ya mara kwa mara wanapoitwa Stars, ikiwamo kuzuiwa na klabu yao hata
katika michezo muhimu ya Kalenda ya Shirikisho la Soka
la Kimataifa (FIFA).
Safari hii kitendo hicho, kiliwaudhi wapenzi na mashabiki wengi wa
soka nchini na kusababisha nyota hao kuzomewa Uwanja wa Taifa, siku
Stars ilipoumana na Zambia.
Stars inaingia kambini ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mchezo wa
kuwania kufuzu kwa
Fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Morocco
utakaochezwa Machi mwaka huu.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
Boniface Wambura, Kocha Poulsen amewateua wachezaji hao ambao wataripoti
kambini Januari 7, katika hoteli ya Tansoma saa 11.30 jioni.
Wambura aliwataja nyota hao na klabu zao kwenye mabano kuwa ni makipa
Juma Kaseja (Simba), ambaye pia ndiye nahodha, Aishi Manula na Mwadini
Ally (Azam), mabeki Aggrey Morris, Erasto Nyoni (Azam), Issa Rashid
‘Baba Ubaya’ (Mtibwa Sugar), Kelvin Yondani, Nadir Haroub ‘Canavaro’
(Yanga), Shomari Kapombe, Amir Maftah (Simba).
Viungo ni Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Khamis Mcha ‘Viali’ (Azam), Amri
Kiemba, Mwinyi Kazimoto (Simba), Athuman Idd ‘Chuji’, Frank Domayo
(Yanga), na Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), huku washambuliaji ni John
Bocco (Azam), Mbwana Samata, Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DRC), Mrisho
Ngasa (Simba), na Simon Msuva (Yanga).
Wambura alilitaja benchi la ufundi mbali na Poulsen kuwa ni Sylvester
Marsh (Kocha Msaidizi), Juma Pondamali (Kocha wa makipa), Leopold Tasso
(Meneja), Dk. Mwanandi Mwankemwa (Daktari wa timu), Frank Mhonda
(Mtaalamu wa tibamaungo), na Alfred Chimela (Mtunza vifaa).
No comments:
Post a Comment