KIKOSI cha Usalama Barabarani Nchini, kimetangaza kuanzisha
vituo maalumu vya ukaguzi wa mabasi ya abiria badala ya utaratibu
inaoutumia sasa wa kuyakagua kila sehemu.
Hatua hiyo ilitangazwa juzi usiku jijini Dar es Salaam na Kamanda wa
Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Nchini, Mohamed Mpinga, wakati
akizungumza katika Televisheni ya Taifa (TBC).
“Tuna mikakati minne tuliyojiwekea kwa mwaka 2013; tuna mpango wa
kufanya ukaguzi kwa mabasi ya abiria kwa kuweka vituo maalumu badala ya
kuyasimamisha kila sehemu. Kwa kaskazini tutaweka pale Same, kwa kwenda
njia ya kati tutaweka Singida na kwenda kusini tutaweka kituo mkoa wa
Iringa,” alisema Kamanda Mpinga.
Alieleza kuwa kwa mwaka huu wamejipanga ipasavyo kuboresha mifumo ya
utendaji kazi eneo ambalo litahusisha ukaguzi wa magari kwa lazima
ambapo magari hayo yatakaguliwa kwa kina.
Alisema kwa sasa wapo katika mchakato wa kutumia vifaa vya Wakala wa
Ufundi na Umeme (Temesa) na Chuo cha Usafirishaji (NIT) ili kufanikisha
hilo wamekuwa wakifanya mazungumzo mbalimbali na wadau hao ili
kufanikisha matumizi ya vyombo hivyo.
Jingine ni kufanya utambuzi wa maeneo hatarishi kama mbinu za
kupunguza ajali za barabarani akatolea mfano kwa mkoa wa Pwani ambao
waliufanya kama eneo la mfano kwa kuweka vidhibiti mwendo kasi na
mafanikio wameyaona.
Alisema hatua hiyo imewezesha ajali kwa mkoa wa huo kupungua kwa
asilimia 37, vifo kwa asilimia 57 na majeruhi kwa asilimia 48
ikilinganishwa na mwaka juzi.
No comments:
Post a Comment