WAKATI kikosi cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom,
Simba SC kimewasili jijini Arusha jana, mahasimu wao wa jadi, Yanga
wameendelea kujifua jijini Dar es Salaam.
Simba ipo Arusha tayari kwa mchezo wake wa ligi hiyo dhidi ya
wenyeji, maafande wa JKT Oljoro, utakaopigwa leo kwenye dimba la
Sheikh Amri Abeid.
Aidha Yanga ambao ni vinara wa ligi hiyo hivi sasa, wameendelea na
mazoezi yao kwenye Uwanja wa Mabatini, Kijitonyama na wanatarajiwa
kushuka kwenye Uwanja wa Taifa Jumatano ijayo kuivaa African Lyon.
Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel
Kamwaga, alisema kwamba kikosi cha wachezaji 20 kiliondoka jana asubuhi
kwenda mjini Arusha.
Hata hivyo, Kamwaga hakuwa tayari kutaja majina ya wachezaji
waliokwenda ama kubaki jijini Dar es Salaam bila sababu ya msingi.
Kwa upande wa Yanga, chini ya kocha wake Ernest Brandts, wachezaji
wake wote isipokuwa wale wa kimataifa waliokwenda kwao kuzichezea timu
zao za taifa, jana asubuhi walifanya mazoezi ya kawaida.
Wachezaji wa kigeni wa Yanga waliokwenda kuzitumikia timu zao za taifa
ni pamoja na Haruna Niyonzima (Rwanda) na Hamis Kiiza (Uganda), huku
wale wa hapa nchini waliokuwa kwenye kikosi cha Stars pia walifanya
mazoezi.
Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, alisema jana kwamba kikosi
chote cha Yanga kiko katika hali nzuri na hakuna majeruhi yeyote.
No comments:
Post a Comment