Jeshi la Ufaransa nchini Mali sasa linaripotiwa kufanya mashambulizi ya
anga dhidi ya maghala ya mafuta na kambi za vikundi vya Waislamu wenye
msimamo mkali huko kaskazini mwa Mali.

Akizungumza kupitia radio moja ya Kifaransa, Waziri wa Mambo ya Nje wa
nchi hiyo, Laurent Fabius, amesema usiku kucha kuamkia leo ndege za
kivita zimeshambulia mkoa wa Kidal, uliyopo mpakani mwa Mali na Algeria.
Amesema hatua hiyo ni moja kati ya malengo makubwa ya kuweza kukata
uwezo wa kujipatia mahitaji yao muhimu kwa kundi hilo ambalo lilidhibiti
sehemu kubwa ya eneo hilo na kushinikiza sheria kali kwa wakazi wa
maeneo hayo.
Aidha Fabius amesema kwa mashambulizi hayo waasi hao hawawezi kuendelea
kudumu kuishi kwa muda mrefu katika eneo hilo, labda wawe na hazina mpya
ya mahitaji yao. Ufaransa iliingia nchini Mali, Januari 11 kwa lengo la
kuwazuia kusonga mbele kundi la waasi la Ansar Dine lenye mafungamano
na al-Qaida.
Vikosi vya Mali na Ufaransa mjini Gao
Fabius amerejelea msimamo wa nchi yake wa kutaka jeshi la
Afrika kuchukua haraka kwa kadri iwezekanavyo dhamana ya ulinzi katika
mji wa kihistoria wa Timbuktu. Kwa sasa, Ufaransa inadhibiti mji huo na
mingine kadhaa tangu ianze operesheni hiyo.
OIC kuzungumzia ghasia za Mali
Wakati mapigano yakiendelea nchini Mali, viongozi wa Jumuiya ya Mataifa
ya Kiislamu, OIC, wanatarajiwa kukutana mjini Cairo, Misri, ambako
pamoja na mgogoro wa Syria, suala la Mali litapewa nafasi. Taarifa
zinaeleza kuwa mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa hayo wanaanza kikao
cha maandalizi leo hii. Mkutano huu mkubwa utawakutanisha viongozi 26
kati ya mataifa 57 ya OIC.
Viongozi wa OIC walipokutana mjini Makka
Rais Mohamed Morsi wa Misri safari hii anatarajiwa kuchukua
uongozi wa umoja huo ambao kwa kawaida nafasi yake inatolewa kwa zamu
kwa nchi wanachama. Katibu Mkuu wa OIC, Ekmeleddin Ihsanoglu, amesema
mkutano huu wa sasa ulipaswa kufanyika mwaka 2011 lakini uliaharishwa
baada ya kutokea vuguvugu la mageuzi katika mataifa ya Kiarabu na
kuwaondoa watawala wanne wa kiimla akiwemo Hosni Mubarak wa Misri.
Mwanadiplomasia huyo wa zamani ya Kituruki amesema mkutano huo wa kilele
utajadili migogoro mikubwa katika mataifa ya Kiislamu. Aidha ameonesha
kusikitishwa kwake na migogoro sambamba na kasi ya vikundi vyenye
misimamo mikali ya Kiislamu ukiwemo huu unaofukuta sasa wa Mali. Tofauti
za sera za mambo ya nje na kusaidiana kwa nchi wanachama wa jumuiya
hiyo, ni miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa katika mkutano huo wa
kilele wa siku mbili.
No comments:
Post a Comment