MBWANA
Samatta, mshambuliaji wa timu ya taifa ya Tanzania anayecheza soka la
kulipwa katika klabu ya TP Mazembe ya Lubumbashi, DR Congo, alitumia
vizuri pasi iliyotoka kwa Frank Domayo na kuukwamisha mpira wavuni
dakika ya 90.
Bao
hilo lilitokana na makosa ya kipa wa Cameroon, Komguep aliyeruka juu
kutaka kuokoa mpira huo, lakini ukatua miguuni mwa Samatta na
kuusindikiza wavuni.
Katika
mchezo, Taifa Stars walianza kwa kasi na kulishambulia lango la
Cameroon, dakika ya nne walifanikiwa kulifikia lango la wapinzani wao,
lakini walishindwa kujipatia bao la haraka.
Ndani
ya dakika saba ya kipindi cha kwanza, mshambuliaji wa kimataifa wa
Taifa Stars, Mbwana Samatta, alichezewa vibaya mara tatu.
Wakicheza
kwa kuonana vizuri, Frank Domayo na Abubakari ‘Sure Boy’, waliweza
kuwasumbua viungo wa Cameroon dakika ya 12, huku kipa Juma Kaseja akiwa
mapumziko.
Cameroon
walipata nafasi nzuri ya bao, kufuatia mpira wa kona, lakini beki
kisiki wa Stars, Kelvin Yondan aliondoa hatari hiyo langoni kwao.
Dakika
ya 14, Kaseja alipata maumivu kidogo baada ya kuangukiwa na
mshambuliaji wa Cameroon, Tchami Herve, lakini baada ya kutibiwa
aliendelea kukaa langoni.
Cameroon
walifanya shambulizi la nguvu dakika ya 24, lakini shuti kali la Tchami
lilitoka nje kidogo ya lango la Stars, huku Kaseja akiwa amesimama bila
ya kujaribu kuufuata mpira.
Mashambulizi
ya Stars yalifanikiwa kuwachanga mabeki wa Cameroon na kuzaa penalti
baada ya beki mmoja wa timu hiyo kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari
na mwamuzi Munyemana Hundu kutoka Rwanda kupuliza filimbi ya adhabu
hiyo.
Beki wa Stars, Erasto Nyoni, alikosa penalti hiyo baada ya kipa wa Cameroon, Effala Komguep, kuudaka mpira huo.
Stars
walikianza kipindi cha pili kwa kuliandama lango la wapinzani wao,
ambapo dakika ya 49, lakini krosi ya Nyoni ilitoka nje ya lango.
Stars
wakicheza soka safi na kuwafanya Cameroon, washindwe kumfikia kipa Juma
Kaseja, kwa muda wa dakika 29, wakati dakika ya 78, Thomas Ulimwengu
alishindwa kuunganisha vizuri kwa kichwa mpira wa krosi uliopigwa na
Mbwana Samatta.
Kwa
ushindi huo, Stars itakuwa inajitengenezea nafasi kubwa ya kuombwa
mechi za kirafiki na nchi nyingine zilizo bora katika soka barani
Afrika.
Mwanzoni
mwa mwaka huu, Stars ilifanikiwa kuwachapa mabingwa wa Mataifa ya
Afrika mwaka jana, Zambia ‘Chipolopolo’, bao 1-0, bao lililofungwa na
Mrisho Ngassa.
Matokeo
hayo ndiyo yaliyowavutia Cameroon, mpaka wakaomba kucheza mechi ya
kirafiki na Stars, hivyo baada ya kipigo cha leo, itakuwa imepanua wigo
zaidi wa mataifa mengine kuomba mechi ya kirafiki.
Stars:
Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Kelvin Yondan, Aggrey
Morris, Salum Abubakari ‘Sure Boy’, Mrisho Ngassa, Frank Domayo, Mbwana
Samatta, Mwinyi Kazimoto/Thomas Ulimwengu, Amri Kiemba.
Cameroon:
Effala Komguep, Assout Ekotto, Aminou Bouba, Ngoula Patrick, Nyom
Allan, Pierre Wome, Kiunge Mpondo, Benino Henry, Tchami Herve/Elounu,
Olinga Fabrice, Aboubakar Vincent.

No comments:
Post a Comment