KAMPUNI ya Msama Promotions ya jijini Dar es Salaam chini ya Mkurugenzi wake, Alex Msama, imepanga kutumia sh milioni 200 katika Tamasha la Pasaka la mwaka huu litakalofanyika mikoa saba tofauti.
Kwa mujibu wa Msama ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, fedha hizo zitatumika kwa masuala mbalimbali ikiwamo kuwalipa wasanii, misaada katika masuala ya kazi za kijamii na gharama za kawaida mahali watakapofanya maonesho.
“Kila mwaka Tamasha la Pasaka linafanyika katika mikoa miwili, kwa maana ya Dar es Salaam na mkoa mwingine tutakaouchagua, lakini mwaka huu kwa mara ya kwanza litafanyika mikoa saba.
“Kwa hiyo, gharama zake kidogo zitaongezeka na tunakadiria kwa mikoa yote hiyo kiasi cha sh milioni 200 zitatumika, maana tutakuwa na wasanii zaidi ya 30, tunaamini wengi watajumuika nasi kulipa viingilio ili kuwezesha dhamira yetu ya kupeleka ujumbe kwa njia ya muziki ufike,” alisema Msama.
Alisema tayari wamekubaliana Machi 31 mwaka huu ambayo ni Siku ya Pasaka, tamasha lifanyike Dar es Salaam, lakini baada ya hapo mikoa mingine itakayofuata wataitangaza.
Msama alisema dhamira yao safari hii kwenye tamasha hilo ni kuhamasisha umoja, amani na mshikamano miongoni mwa jamii ya Kitanzania.
“Kila mwaka huwa tuna jambo ambalo tunaliangazia, safari hii tumeamua kuwa tamasha letu litasisitiza amani na upendo,” alisema Msama.
Baadhi ya waimbaji mahiri waliokuwapo mwaka jana ni Rose Muhando, Rebecca Malope, Christina Shusho, Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, Solomon Mukubwa, Atosha Kissava, Ephraim Sekeleti, kundi la Glorious Celebration, kwaya mahiri ya Kinondoni Revival na Mwinjilisti Faraja Ntaboba kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
No comments:
Post a Comment