Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC imefuta kesi iliyokuwa
ikimkabili mkuu wa zamani wa utumishi wa umma nchini Kenya, Francis
Muthaura kwa madai ya kukosekana ushahidi wa kutosha.
Mwendesha mashtaka wa ICC, Bi. Fatou Bensouda amesema mashahidi
muhimu kwenye kesi hiyo wamejiondoa na hivyo kudhoofisha kesi yenyewe.
Muthaura alikuwa akikabiliwa na tuhuma za kuhusika na ghasia za baada ya
uchaguzi mkuu wa mwaka 2007. Francis Muthaura alikuwa miongoni mwa
Wakenya 4 wanaokabiliwa na kesi za jinai dhidi ya binadamu mbele ya
mahakama hiyo yenye makao yake mjini Hague, Uholanzi.
Mkuu huyo wa zamani wa utumishi wa umma alikuwa kwenye kundi moja na
Rais Mteule, Uhuru Kenyatta. Watuhumiwa wengine ni Makamu wa Rais
mteule, William Ruto pamoja na mtangazaji wa radio, Joshua Arap Sang.
Kesi ya Sang na Ruto inatarajiwa kuanza mwezi Mei huku ile ya Kenyatta
ikitarajiwa kuanza mwezi Julai mwaka huu.
Weledi wa mambo wanasema huenda ikawa vigumu kwa Kenyatta na Ruto
kuhudhuria vikao vya ICC hasa baada ya kuchaguliwa Rais na Makamu wa
Rais siku chache zilizopita.
No comments:
Post a Comment