UMOJA wa wakusanyaji na wauzaji wa samaki katika Soko la Ferry
(Uwasau), umesema hautakubali kulipa ushuru wa asilimia tano hadi
mgogoro wao utakapopatiwa muafaka na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na
Uvuvi, Dk. Mathayo David.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa
wiki, kiongozi wa umoja huo, Abed Seleman, alisema hadi sasa hakuna
utaratibu wa kisheria unaoeleweka unaotumiwa na viongozi wa soko hilo
katika kukusanya ushuru.
Alidai kuwa wafanyabiashara sokoni hapo wamegeuzwa mtaji na baadhi ya
watendaji wa soko hilo kwa kulazimishwa kulipa ushuru, huku wakiambiwa
kuwa hawako kisheria katika eneo wanalofanyia biashara.
“Sisi si wavuvi, hivyo kututoza ushuru kama wavuvi, hatukubali, kwani hawatutendei haki,” alisema.
Aidha, alisema hawapingi mipango ya serikali ya kusimamia vyanzo
vyake vya mapato, bali wanapinga ubabe wanaofanyiwa na watendaji hao kwa
kulazimishwa kulipa ushuru huku wakinyimwa baadhi ya huduma katika eneo
wanalofanyia kazi.
Kwa upande wake, Katibu wa soko hilo, Mbaraka Kilima, alisema suala
linalowakabili wafanyabiashara hao ni la kisheria zaidi, ambapo sheria
imefafanua kuwa eneo wanalofanyia biashara si rasmi.
Alisema wafanyabiashara hao hawana ujanja bali wanachotakiwa ni kutii
sheria kama inavyowaelekeza kuuza samaki wao katika eneo la mnada ambalo
limetengwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za uendeshaji wa soko hilo.
No comments:
Post a Comment