JAMII imetakiwa kuokoa watoto wa kike kutoka katika mazingira duni yanayowafanya wanyanyasike na kukosa haki za msingi.
Wito huo ulitolewa juzi na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudencia Kabaka,
wakati akizindua kampeni ya ‘Okoa Mtoto wa Kike Tanzania’ iliyofanyika
mjini Nyamongo wilayani Tarime.
Alisema watoto wa jinsia ya kike wanaolelewa kwa kupewa fursa ya
kupanua ubongo, wanakuwa na maendeleo mazuri kuliko wanaokua katika
manyanyaso na kufanywa hawawezi kila jambo au mambo fulani.
Alisema mila za makabila ya Mkoa wa Mara hususan wilayani Tarime,
mtoto wa kike anaandaliwa kuolewa, kwa kuwa hawaoni sababu ya kumpatia
elimu, zinachangia kumfanya aishi katika hali duni, manyanyaso na
utumwa.
Alisema utafiti uliofanywa hivi karibuni unaonesha kuwa asilimia 51 ya
wanawake wanaoolewa hunyimwa haki ya ardhi, na watoto mara
wanapotengana na waume huku asilimia 30 wakinyimwa urithi.
Awali, akisoma risala kwa Waziri Kabaka, Mkurugenzi wa Nyumbani Kwanza
Media Group, Mossy Magere, alisema lengo la kuandaa kampeni hiyo ni
kutaka kujikita katika kuwaelezea jamii umuhimu wa mtoto wa kike na
kwamba kampeni hiyo imedhamiria kufanya mambo ya kijamii zaidi.
Alisema kuwa kutokana na umuhimu wa tamasha hilo, wadau wengi
wamejitokeza kusaidia akiwamo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na
Madini, Eliakimu Maswi, mjumbe wa NEC ya CCM Wilaya ya Tarime,
Christopher Gachuma na Kampuni ya Barrick kupitia mgodi wa North Mara.
No comments:
Post a Comment