Umoja wa Ulaya umezionya nchi wanachama wa Umoja huo kuweka mikakati
imara dhidi ya biashara ya kuuza binaadamu isiokubalika au ziwekewe
vikwazo.
Ripoti ya halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya, imesema tangu mwaka wa 2008
hadi mwaka wa 2010 biashara ya kuuza watu imeongezeka kwa asilimia 18
katika mataifa 27 yanayounda Umoja wa Ulaya.
Kulingana na kamishna anayeshughulika na maswala ya jamii katika Umoja
huo Cecilia Malmstroem, Wanawake wanaume na watoto wanaendelea kuuzwa
katika biashara ya ngono, kazi ngumu, ndoa za kulazimishwa, kazi za
nyumbani, kuomba au hata kutolewa sehemu zao za mwili kwa ajili ya
biashara. "Huu ni ukweli unaouma," alisema kamishna Malmstroem.
Kamishna wa Umoja wa Ulaya katika maswala ya Jamii Cecilia Malmstroem
Utafiti uliofanywa mwezi Juni mwaka jana na shirika la kazi
duniani, ulikadiria takriban watu 880,000 walilazimika kufanya kazi
ngumu katika mataifa ya Ulaya, jambo ambalo linatarajiwa kuongezeka
kutokana na mgogoro wa uchumi, unaoshuhudiwa kwa sasa katika baadahi ya
nchi, kwasababu raia katika nchi hizo hutafuta ajira za aina yoyote ile
ili waweze kujikimu kimaisha.
Ripoti hiyo iliotolewa jana imeonesha watu 7 kati ya kumi wanaouzwa ni
wanawake, asilimia 17 ya wanaume, asilimia 12 ya wasichana huku asilimia
3 ikiwa ni ya watoto wadogo wa kiume. zaidi ya nusu ya waathiriwa yani
asilimia 61 wanatokea katika mataifa ya Umoja wa Ulaya hasa Romania na
Bulgaria wakati Nigeria na China ni katika mataifa yanayojulikana sana
kwa jambo hilo nje ya bara la ulaya.
Kamishna Cecilia Malmstroem amesema japo ripoti ilionesha kukamatwa kwa
wanaoendesha biashara za kuuza watu, mataifa mengi ya Umoja wa Ulaya
yameshindwa kutekeleza mikakati thabiti dhidi ya biashara hiyo, mikakati
ambayo ilikubalika mwaka uliopita.
Mataifa machache yatekeleza mkakati wa EU
Kati ya nchi 27 ni nchi 6 tu zilizotilia maanani mikakati hiyo iliowekwa
na Umoja wa ulaya. Nchi kama Jamhuri ya Czech, Finland, Latvia,
Hungary, Poland na Sweden ndizo zilizo tekeleza hatua hiyo huku
Ubelgiji, Lithuania na Slovenia zikionekana kutaka kuchukua mwelekeo
kama huo.
Wanafunzi Romania wakionesha athari za biashara ya kuuza watu
Sasa Umoja huo umetaka kila nchi kutilia manani kuweka sheria
ya kudhibiti biashara hiyo au iwekewe vikwazo. Bara la Ulaya miaka
miwili iliopita ilikubali kusimama kidete dhidi ya biashara hiyo
inayokadiriwa kuingiza euro bilioni 2.5 kila mwaka kwa kupanua ufafanuzi
juu ya uhalifu huo na kulenga masuala ya ngono, kazi ngumu, kuomba na
kutolewa kwa sehemu za mwili na kuweka sheria kali za kuendana na hilo.
Mikakati hiyo mipya inajumuisha miaka mitano kwa atakayepatikana na
makosa na miaka kumi kwa kosa lolote litakalojumuisha utumiaji wa watoto
au mateso au uhalifu. Hatua nyengine ni kukubalika kwa mataifa hayo
kuchukua uamuzi wa kimahakama nje ya nchi yake katika tukio ambalo
limetendwa na raia wa nchi yake au mkaazi wa nchi hiyo.
Hata hivyo Utafiti uliofanywa na shirika la kazi duniani mwaka 2012,
ulionesha watu milioni 21 duniani kote ni waathirika wa biashara hii ya
kuuza watu isiokubalika.
No comments:
Post a Comment