Juu na chini anaonekana Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini ya Kikristo Ikulu jijini Dar es salaam jana ambapo amekuwa na mazungumzo nao ikiwa ni mojawapo ya jitihada za Rais Kikwete kutafuta muafaka na kutafuta utatuzi wa hali ya sintofahamu ambayo
inanyemelea nchi yetu katika kipindi hiki.
 
 Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika mazungumzo na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini ya Kikristo Ikulu jijini Dar es salaam jana.

Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete katika picha ya pamoja na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini ya Kikristo Ikulu jijini Dar es salaam jana. Kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano) Mhe Steven Wassira.
************************************ 

Viongozi hao wa dini wamemueleza Rais Kikwete kuwa wanaunga mkono jitihada zake za kutafuta amani na kwa pamoja wamekubaliana uandaliwe mkutano wa pamoja baina ya viongozi wa dini zote ambapo masuala ya amani na umoja wa nchi utajadiliwa kwa kirefu.

Katika kikao cha jana pande zote zimekubaliana kuwa kuna changamoto zilizoko sasa zinahitaji kutatuliwa haraka iwezekanavyo ili kuepusha nchi kutumbukia katika mgogoro mkubwa zaidi, na pia kukubaliana kuwa pande zote, kwa maana ya serikali na taasisi za dini, zinawajibu mkubwa wa kuhakikisha amani inadumu.

Kabla ya kikao cha jana , Rais amewahi kukutana na viongozi wa dini ya kiislamu na kikristo mmoja mmoja ambapo alikua akitafuta maoni na ushauri wa pande zote kabla ya pande zote hazijakaa pamoja na kuwa na msimamo wa pamoja.
Kikao cha leo kimehitimisha jitihada hizo na kinachofuata ni mkutano mmoja ambapo Rais Kikwete atakutana na viongozi wa dini zote kwa pamoja hivi karibuni.
Imetolewa na:
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi,
Ikulu-DSM
23 Aprili, 2013
Chanzo Mo Blog.