WAREMBO 14 kutoka vitongoji vitano vya wilaya za Siha na Hai,
Kilimanjaro, akiwemo mdogo wake Wema Sepetu, wamejitokeza kushiriki
shindano la kumsaka mrembo wa Hai, ‘Redds Miss Hai 2013.
Shindano hilo linalotarajiwa kulindima Hoteli ya Snow View Bomang’ombe Hai, Ijumaa.Akizungumza mjini hapa jana, muandaaji wa mashindano
hayo, Grace
Mmari, kupitia kampuni ya ulinzi ya FEM ya jijini Arusha,
alisema maandalizi ya mashindano hayo yamekamilika na tayari warembo hao
wako kambini kwa wiki mbili sasa katika hoteli ya Sinza B.
Alisema warembo hao wamepatikana kutoka vitongoji vya Kwa Sadala,
Bomang’ombe, Sanya Juu, Machame na KIA, ambao wana vigezo vyote huku
akitamba mwaka huu, Mrembo wa Tanzania atatoka wilaya ya Hai.
“Warembo wangu ni wazuri, warefu, wanajiamini na wana uwezo wa
kuwakilisha vyema wilaya ya Hai, mkoa wa Kilimanjaro na hata taifa, kwa
kuwa tunao kina Wolper wengine hapa na kina Sepetu wapo pia,“ alisema.
Alisema miongoni mwa warembo waliojitokeza kushiriki shindano hilo ni
pamoja na mdogo wa mrembo wa zamani wa Miss Tanzania (2006), Wema
Sepetu, Weru Sepetu, ambaye alidai kuwa huenda akafuata nyayo za dada
yake.
Aliwataja warembo watakaoshiriki shindano hilo kuwa ni Sharon Abdalah,
Zena Ally, Ivony Steven, na Winny Shayo wanaotoka Machame na Sanya Juu.
Wengine ni Julieth Kimaro, Rehema John, Mary Chemponda, Catherine Leonard na Modesta Joseph.
Mmari alisema shindano hilo litapambwa na msanii wa muziki wa kizazi
kipya, Rich Mavoko pamoja na Jambo Squad, ambako mgeni rasmi anatarajiwa
kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Novatus Makunga.
Kwa upande wake, mwalimu wa warembo hao, Evameri Gamba, alisema
warembo wanaendelea na mazoezi ya mwisho pamoja na kushiriki shughuli
mbalimbali za kijamii, ikiwemo uoteshaji wa miti na kutembelea wagonjwa
katika hospitali ya wilaya ya Hai.
Shindano hilo linafanyika kwa mara ya pili sasa, huku wadhamini wakiwa
ni TBL kupitia kinywaji chake cha Redds, Fem Security, Bonite Bottlers,
Snow View Hotel, Panone pamoja migodi ya madini ya Anglo America Mining
na Manga Germ.
No comments:
Post a Comment