Dar es Salaam
Azam FC inashuka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
leo kuivaa Barrack Young Controllers ya Liberia katika mchezo wa
marudiano wa Kombe la Shirikisho, huku ikiwa na faida ya mabao mawili
iliyopata ugenini katika mchezo wa kwanza.

Pamoja na kumbukumbu hiyo nzuri ya ushindi wa ugenini, bado Azam wana
kazi kubwa ya kufanya kuweza kuitoa nje ya mashindano timu hiyo ya Liberia ambayo hakuna shaka imepania kulipa kisasi.
Kuwasili kwake kwa mapema takriban wiki moja kabla
ya mchezo wenyewe, kunathibitisha kwamba haikuja nchini kutalii zaidi
ya kusaka ushindi.
Kocha wa Azam Stewart Hall atategemea huduma ya mshambuliaji wake aliyepona, Brian Umony ili ashirikiane na John Bocco katika kutumbukiza mabao kwenye wavu wa Barrack.
Pia anakusudia kumrejesha katika sehemu ya kiungo
wa juu, Salum ‘Sure Boy’ Abubakar’ ambaye hakuwapo kwenye mchezo wa
kwanza ili kusuka mipango ya mabao sambamba na Kipre Bolou.
Akizungumzia kipute hicho, Hall alisema kikosi chake kimeiva vya kutosha na kipo tayari kuingia uwanja wa mapambano na kuhakikisha jahazi la Barrack linazama.
“Nimewaambia wachezaji wangu, tuache kufikiri
kuhusu ushindi wetu wa mabao 2-1, tunatakiwa kupigana mpaka mwisho na
ndivyo tutakavyofanya leo,” alisema Hall.
Naye kocha wa timu ya Barrack YC II, Robert
Lartely amesema kuwa wamekuja kushinda na siyo kusindikiza licha ya
kukoseshwa usingizi na wachezaji watatu wa Azam.
Lartely alisema wachezaji wanaomumiza kichwa ni Kipre Tcheche, Ibrahimu Mwaipopo na John Bocco ‘Adebayor’.
“Ni wachezaji wanaotutisha sana, tuliwaona Liberia lakini tumejipanga kushinda, hakuna shaka dhamira yetu itatimia,” alisema Lartely.
Alisema wamejipanga kuhakiksha wanawadhibiti wachezaji hao ili wasilete madhara.
Alisema kikosi chake kilichowasili mapema wiki
hii, hakina majeruhi na kwamba wachezaji waliocheza kwenye mechi ya
awali nchini Liberia watacheza.
“Asilimia kubwa tutatumia wachezaji wale wale
waliocheza mechi ya mwanzo, kama kuna mabadiliko ni madogo sana. Nina
imani na marekebisho niliyofanya,” aliongeza.
No comments:
Post a Comment