CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kiko kwenye mkakati kabambe wa
kuhakikisha Bunge linapitisha bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha
2013/14.
Kesho Waziri wa Fedha na Uchumi, William Mgimwa, pamoja na Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira,
wanatarajiwa kuhitimisha kujibu hoja za wabunge kisha Bunge kupiga kura
za kuipitisha.
Kwa mara ya kwanza, katika historia ya vyama vingi, bajeti ya
serikali haikujadiliwa na wabunge wa kambi rasmi ya upinzani ya CHADEMA
kutokana na kutokuwapo bungni kwa wiki nzima.
CHADEMA ambao walihamia jijini Arusha kwa ajili ya mazishi na
maombolezo ya wafuasi wao waliouawa kwenye mlipuko wa bomu Jumamosi
iliyopita, waligoma kuwasilisha hata bajeti yao mbadala bungeni.
Hatua ya kutowasilisha mezani hati ya msemaji mkuu wa kambi hiyo kwa
Wizara ya Fedha, Kabwe Zitto, kwa mujibu wa kanuni za Bunge inamaanisha
kuwa hotuba yao hiyo haikuingizwa kwenye rekodi rasmi za Bunge
‘hansard’.
Ijumaa wiki hii, Spika wa Bunge alitangaza kufunga mjadala wa
wachangiaji wa bajeti hiyo, akisema kuwa wabunge waliokuwa wameomba
kuchangia wote walipata nafasi isipokuwa wale walioomba lakini wakapata
dharura.
Kwa mantiki hiyo, CHADEMA ni kwamba hawakushiriki kwa lolote katika
bajeti kuu ya serikali, iwe kwa kupitia maoni ya kambi au mchango wa
mbunge mmoja mmoja.
Kutokuwapo kwa CHADEMA wiki nzima, kumeleta mdororo bungeni kutokana
na mjadala kuegemea upande mmoja wa wabunge wa CCM, japo wabunge wote
watano wa NCCR-Mageuzi na wachache wa CUF walijitahidi kutoa michango
ya kusisimua.
Wabunge machachali wa CCM, Deo Filikunjombe wa Ludewa, Kangi Lugola
wa Mwibara nao hawajaonekana bungeni zaidi ya wiki na vile vile Mbunge
wa Kisesa, Luhaga Mpina na Ali Keissy wa Nkasi Kaskazini wamepinga
bajeti hiyo.
Hali hiyo ni kama imemtisha Spika wa Bunge, Anne Makinda na kuanza
kutilia shaka kuwa huenda bajeti hiyo ikakwama kupitishwa kutokana na
idadi ya wabunge kutotimia.
Akiahirisha Bunge juzi, Spika aliwataka wabunge wote kuhakikisha
wanahudhuria Bunge kesho, huku akiwahimiza mawaziri walioko safarini au
wale wanaokusudia kusafiri wasitishe safari hizo hadi bajeti hiyo
itakapokuwa imepitishwa.
Hatua ya CHADEMA kutoshiriki mjadala wa bajeti, bado inatia hofu kama
wabunge hao kesho wataingia bungeni wakati wa kuipitisha bajeti hiyo.
Katika maelekezo yake juzi, Spika Makinda alilazimika kuwasomea
wabunge kanuni kuhusu nini kitatokea endapo bajeti hiyo kuu ya serikali
itashindwa kupita.
Bila kufafanua vizuri kusudio lake, Makinda alisema anawakumbusha tu
ili wafahamu kuwa idadi yao isipotimia bajeti hiyo haiwezi kupita na
kwamba hali hiyo ikitokea mara tatu Rais atalivunja Bunge.
Alisema utaratibu unaotumika kwenye kupitisha bajeti za wizara ni
tofauti na ule wa bajeti kuu kwani wakati wa kupiga kura kila mbunge
anaitwa kwa jina kisha anasema kama anaiunga mkono au anaikataa.
CCM katika kuhakikisha bajeti hiyo inapitishwa, wabunge wake wengi
wamekuwa wakiipigia debe na kuwashawishi wenzao waiunge mkono ili fedha
zilizoidhinishwa kwa wizara ziweze kutolewa haraka.
Katika kuwekana sawa, Katibu wa wabunge wa CCM, Jenista Mhagama,
aliitisha kikao cha wabunge hao jana saa tano katika ukumbi wa Msekwa
mjini hapa.
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa kikao hicho ni kwa ajili ya
wabunge hao kujipanga kuiunga mkono bajeti hiyo ili ipitishwe na idadi
inayotakiwa hata kama wabunge wa upinzani na wale wachache wa CCM
wasipoiunga mkono.
Via Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment