SAKATA la kupigwa kwa Katibu wa Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu
nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda, limezidi kuitesa serikali, safari hii
Tume ya Haki na Jinai ya Jeshi la Polisi chini ya Mwenyekiti Kamishina
wa Jeshi hilo Isaya Mngulu iliyoundwa kuchunguza kujeruhiwa kwake
ikikwaa kisiki.
Jana wajumbe wa tume hiyo, walitimuliwa jijini Dar es Salaam na huko
Morogoro walipokwenda kufanya mahojiano na baadhi ya viongozi na wafuasi
wa kiongozi huyo.
Jijini Dar es Salaam tume hiyo ilitimuliwa kufuatia maofisa wake
kushindwa kujitambulisha wakati wakitaka kumhoji Sheikh Ponda katika
Hospitali ya Muhimbili alikolazwa.
Taarifa ya kutimuliwa kwa maofisa wa tume hiyo ilitolewa jana jijini
Dar es Salaam na Is-haq Rashid, msemaji wa familia ya Sheikh Ponda,
wakati akiongea na waandishi wa habari.
Is-haq alisema juzi wakati maofisa hao wanaodaiwa kutoka tume ya haki
jinai ya Jeshi la Polisi walifika katika chumba alicholazwa Sheikh Ponda
pasipo kujitambulisha kama ni maofisa wa tume au askari wanaotaka kujua
ukweli wa tukio la kujeruhiwa kwa kiongozi huyo.
“Walikuja na wakawa wanaongea na Sheikh pasipo kujitambulisha, kwa
bahati nzuri tulimtambua yule Isaya Mngulu na hapo ndipo tukaanza kuhoji
sababu ya ujio wao wa kimya kimya pasipo kututaarifu na hata walipopata
nafasi ya kuongea na mgonjwa pia hawakuweza kujitambulisha nia yao,”
alisema Is-haq.
Aliongeza kuwa kutokana na viashirio hivyo, hawana imani na utendaji
wa tume hiyo na hivyo hawatatambua matokeo yoyote yatakayotolewa kwa
kuwa hayana lengo la kuwashirikisha.
Alisema mwanzoni walidhani polisi walikuwa na nia ya kusaidia kubaini
ukweli wa tukio hilo na kwamba wamebaini dhamira ya jeshi hilo ni
kutafuta njia ya kujisafisha.
Is-haq alisema wao kama familia kwa sasa wameshaanza kukusanya
ushahidi na wakishaukamilisha watatoa taarifa kwa umma juu ya mtu
aliyefanya unyama huo.
Wajumbe wa tume hiyo pia walikwaa kisiki mkoani Morogoro baada ya baadhi ya wafuasi wa Ponda kugoma kutoa maelezo.
Akizungumza na Waislamu waliokuwa wamefurika kituo kikubwa cha polisi
mkoani Morogoro baadae kuhamishiwa msikiti mkuu, Mwenyekiti wa taasisi
hiyo mkoani humo Ayubu Salum Mwinge alisema hawatatoa ushirikiano huo
kwenye tume hiyo kwa kuwa wakosaji ni polisi na haikuwashirikisha wao
kama waathirika wa suala hilo.
“Tume hiyo ni yao na haijatushirikisha kama waathirika wa jambo hili,
baada ya kuvutana kwa muda tumewataka watushirikishe na sisi humo,”
alifafanua Mwinge.
Aliongeza kufafanua kuwa mbali na tume hiyo kuwashirikisha viongozi
kutoka kwa mwanasheria na mkurugenzi wa makosa ya jinai (DPP) hawana
imani nayo kwa kuwa wote ni wajumbe wa serikali.
“Ikumbukwe kuwa hawa wanatekeleza agizo la kiongozi wa serikali la
‘wapigwe tu’. Ni hivi karibuni bungeni Waziri Mkuu Mizengo Pinda
aliwangiza polisi kufanya hivi, sasa sisi tutakubaliana nao kivipi juu
ya tume yao hiyo?
“Nikweli wapo wananchi walioshuhudia tukio zima, lakini hatuwezi
kuwaita kutoa ushuhuda huo kwa kuwa kwanza ni tume ya upande mmoja yaani
polisi, ni wapigaji risasi, na ni wao wachunguzaji,” alisema.
Hivi karibuni Sheikh Ponda akiwa mjini Morogoro kwenye sherehe za Idd
alipigwa na kitu kinachodaiwa kuwa ni risasi na watu wanaodaiwa kuwa
polisi baada ya kumzuia barabarani akielekea kuswali swala ya jioni.
CHADEMA waijia juu polisi
Wakati huo huo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
kimelishambulia Jeshi la Polisi kikisema kuwa haliwezi kukwepa dhamira
ya kutaka kumuua Sheikh Ponda.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Profesa Abdallah Safari akiongea na
waandishi wa habari katika makao makuu ya chama hicho jijini Dar es
Salaam, jana alisema imekuwa ni kawaida ya Jeshi la Polisi kuua watu
hovyo na kisha kutafuta sehemu ya kujificha huku akikumbushia mauaji
mbalimbali yanayodaiwa kufanywa na jeshi hilo kuanzia miaka ya 80.
Miongoni mwa mauaji aliyokumbusha ni pamoja na vifo vya wakata miwa 20
waliouawa mkoani Morogoro mwaka 1980, ambao walikuwa wakidai haki
ambapo kamanda wa polisi wa wakati huo mkoani humo alifukuzwa kazi.
Alisema utendaji wa serikali kwa wakati huu ni tofauti na wakati wa
Mwalimu Nyerere ambaye alimlazimisha IGP Hamza Azizi ajiuzulu nafasi
yake kwa kisa cha kumgonga mtu na kumsababishia kifo.
“Leo wanaosababisha au kusimamia mauaji wanaongezwa vyeo. Mfano ni
mauaji ya mwandishi wa habari Daudi Mwangosi, Kamuhanda ameongezwa cheo
badala ya kuwajibishwa na huu ni mfumo mbovu wa kiutawala,”alisema Prof.
Safari.
Kuhusu Tume ya Haki Jinai ya Jeshi la Polisi, Profesa Safari alisema
CHADEMA haina imani na tume hiyo inayoongozwa na Mngulu kwa kuwa ni
ofisa aliyefanya kazi mbalimbali ikiwemo tukio la bomu la Arusha pasipo
kutoa majibu hadi leo.
Alisema ni wakati wa Watanzania wenye kuitakia mema nchi kuunganisha
nguvu na kuilazimisha serikali kuchukua hatua juu ya maovu yanayofanywa
na watendaji wake kwa raia.
Ponda atuma salamu kwa watetezi wa haki
Akizungumza na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA),
John Heche aliyemtembelea hospitalini hapo jana, Sheikh Ponda alimuomba
kiongozi huyo amfikishie salamu kwa watu wote wenye kutetea haki za
wananchi.
“Nimefurahi… nimefurahi sana mmekuja kunijulia hali naomba nifikishie
salamu zangu kwa wapenda haki wote,” alisema Sheikh Ponda.
No comments:
Post a Comment