UTATA umezidi kuongezeka juu ya tukio la kujeruhiwa kwa Katibu
wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda, baada ya
Kitengo cha Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa na Fahamu
(MOI) kushindwa kubainisha kilichosababisha jeraha hilo.
Hatua hiyo inazidi kuibua maswali kwa vile bado kuna mvutano kati ya
ndugu na wafuasi wa Sheikh Ponda ambao wanadai kuwa alijeruhiwa kwa
kupigwa risasi na askari, wakati Jeshi la Polisi linasisitiza kutohusika
na tukio hilo.
Wakati utata huo ukijitokeza, mashirika ya Utetezi wa Haki za Binadamu
na Baraza la
Waislamu nchini (BAKWATA), wametaka kuundwa kwa tume huru
ya uchunguzi kuhusu tukio hilo huku mashirika hayo yakiahidi kuchangia
rasilimali fedha.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Ofisa
Uhusiano wa MOI,
Almas Jumaa, alisema baada ya Sheikh Ponda kupokewa
juzi alionekana akiwa na jeraha chini ya bega la mkono wa kulia
lililokuwa limeshonwa.
Alisema baada ya uchunguzi wa madaktari walishauriana afanyiwe kipimo
cha X-ray ambacho kilionesha kuwapo kwa mvunjiko bila mifupa kupishana.
“Alipokuja alikuwa ameshafanyiwa tiba ya awali lakini kidonda kilikuwa
katika hali mbaya, tukaona tumfanyie upasuaji mwingine kuzuia
maambukizi,” alisema.
Aliongeza kuwa licha ya kumfanyia upasuaji bado hali ya kubaini kitu
kilichomsababishia jeraha hilo hakijajulikana na kwamba kwa sasa hali
yake inaendelea vizuri.
Akizungumzia tukio hilo, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad
Musa Salum, alisema ni vema serikali ikaunda tume huru ya uchunguzi.
Alisema kuwa pamoja na BAKWATA kupingana na misimamo ya Sheikh Ponda,
bado serikali ilikuwa na nafasi ya kumkamata na kisha kufuata mkondo wa
sheria badala ya hatua ambayo imechukuliwa.
Sheikh Alhad alisisitiza kuwa kabla ya tume hiyo kuanza kazi ni vema
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, akajiuzulu
ili kupisha uchunguzi huru wa tukio hilo.
“Kujiuzulu kwa Kamanda Shilogile ni kwa sababu jeshi limehusishwa na
yeye ndiye msimamizi wa askari katika Mkoa wa Morogoro, ni vema akae
pembeni,” alisema.
Alisema jamii inapaswa kutambua kuwa BAKWATA haina uadui na Sheikh
Ponda, hivyo haiko tayari kuona anadhuriwa kwa namna yoyote.
Mashirika yanena
Akisoma tamko hilo mbele ya waandishi wa habari kwa niaba ya
mashirika hayo, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu,
Onesmo Olengurumwa, alisema uundwaji wa tume hiyo utakuja na majibu
yatakayoweza kuziridhisha pande zote badala ya iliyopo sasa ambayo
imeundwa na polisi wakati wenyewe ni walalamikiwa.
Olengurumwa alisema kutokana na uzoefu walionao na matukio
yanayofanana na hayo, hawana imani kabisa na tume iliyoundwa kwa kuwa
jeshi hilo linatuhumiwa kumjeruhi Sheikh Ponda wakati misingi ya haki za
asili ikiwa haikubaliki mhusika kuwa hakimu kwenye shauri linalomhusu.
Aidha, walitumia fursa hiyo kulaani utaratibu uliotumiwa na polisi
katika kumkamata Sheikh Ponda mbele ya halaiki na wafuasi wake kwa madai
kuwa lilikuwa ni tukio hatarishi kwa askari wenyewe pamoja na maisha ya
raia.
Katika wito wao, mashirika hayo yaliitaka Tume ya Haki za Binadamu na
Utawala Bora ambayo kikatiba ina jukumu la kufuatilia na kuchukua hatua
kwa masuala kama haya ifanye hima kufuatilia na kuchukua hatua zote
stahiki za kisheria.
“Ikiwa tume itahitaji msaada wetu wa rasilimali watu na fedha tuko
tayari ili iweze kufanya kazi hii kwa haraka kama inavyostahili, kwa
kuwa tunaiamini, hasa pale ilipoweza kufanya uchunguzi wake katika
mauaji ya mwandishi wa habari, Daudi Mwangosi na yale ya vurugu za
Arusha, ila changamoto inakuja kwamba huwa inachukua hatua taratibu.
“Pia tunaomba tume hii ifuatilie na matukio mengine mengi ya matumizi
ya nguvu yanayofanywa na vyombo vya dola katika sehemu mbalimbali za
nchi na kwa upande wa wananchi ni vema wawe watulivu na kuzingatia
sheria za nchi katika kudai haki zao,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Utetezi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC), Harold Sungusia, alivitaka vyombo vya dola vianze kujifunza
kutenda haki kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu na utawala bora
na kupendekeza kuwa mfumo wa Jeshi la Polisi uliopo sasa ni vema
ukavunjwa kabla amani haijatoweka, kwa kuwa umekosa mwelekeo.
Katika hili Sungusia alienda mbali zaidi na kutaka kuundwa kwa chombo
kitakachoweza kulisimamia na kuliadhibu jeshi hilo pindi linapokwenda
kinyume cha sheria, kwa kuwa sasa hivi linajifanyia mambo yake likijua
hakuna wa kuliwajibisha.
Akifafanua sheria ambayo inaeleza namna ya kumkamata mtuhumiwa,
alisema kwenye sheria za kesi za jinai mtuhumiwa haruhusiwi kupigwa
risasi, huku akionesha wasiwasi wake kuwa huenda kauli ya ‘piga tu’ ya
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ndiyo ikawa imeanza kutekelezwa.
Mkurugenzi wa Shirika la Sikika, Irenei Kiria, alisema kwa Morogoro
hili tukio si la kwanza, jambo ambalo linaonesha wazi kwamba kuna
uongozi mbovu wa jeshi katika mkoa huo.
Polisi wamkamta
Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova,
alisema kuwa wanamshikilia Sheikh Ponda kutokana na kutuhumiwa kukiuka
masharti ya kifungo anachokitumikia.
Hata hivyo, alifafanua kuwa ulinzi waliomuwekea kwa sasa ni kwa ajili ya kuzuia watu wasiweze kumdhuru.
“Tumesikia matamko mbalimbali yanatolewa, sisi tupo imara kiulinzi na
hatutamvumilia yeyote atakayekwenda kinyume cha sheria hapa Dar es
Salaam, muhimu ni kwamba tunamlinda na kumshikilia Ponda kwa usalama
wake,” alisema Kova.
CREDIT : TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment