MSANII Judith Wambura ‘Lady Jaydee,’ juzi usiku aliubeba
uzinduzi wa filamu ya ‘Foolish Age,’ iliyochezwa na Elizabeth Michael
Lulu uliofanyika Ijumaa usiku katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar
es Salaam.
Jaydee aliyepanda jukwaani baada ya tukio la uzinduzi wa filamu hiyo
akikaribishwa
na Lulu aliyetamka wazi kuwa amekuwa akimpenda Jaydee ‘Anakonda’ tangu
utotoni mwake, aliufanya ukumbi urindime kwa mayowe ya shangwe na
nderemo.
“Napenda kuwashukuru watu wote mliofika hapa Mlimani City katika
uzinduzi wa filamu hii ambayo naamini italishika soko ipasavyo kwa
sababu imechezwa kwa umahiri mkubwa,” alisema Lulu na kuamsha shangwe za
aina yake.
Lulu hakuishia hapo, ndipo akasema atakuwa mchoyo kama asingemtaja
Lady Jaydee aliyekuwa miongoni mwa watu mashuhuri waliofika katika tukio
hilo la historia maishani mwake.
“Lady Jaydee nakupenda sana, njoo dadangu, nilikuwa nakupenda sana
tangu nilipokuwa mdogo hadi sasa bado nakupenda,” sauti ya Lulu
ilisikika ukumbini kupitia kipaza sauti.
Kilichofuata ni Jaydee kwenda jukwaani na moja kwa moja akaanza kuimba
wimbo
wa
‘Njiwa Peleka Salamu’ wa mkongwe Patricia Hillary aliyewainua
mashabiki na kuwaambia wanaruhusiwa kucheza, watu wakaamua kuacha viti
na kwenda kucheza mduara.
Kuanzia hapo, ikawa ni bandika-bandua kwani aliunganisha kibao chake
cha Joto Hasira,’ hivyo kuibua shangwe, nderemo zilizoambatana na mbinja
kiasi cha kuufanya ukumbi kuzizima kabla ya kuongeza kibao cha Yahya.
Wakati akiimba vibao hivyo, wapenzi na mashabiki walishindwa kutulia
kwenye viti vyao na kwenda kumtunza noti zisizo na idadi hadi kulazimika
kusimama kwa muda akusanye kwanza fedha zake kabla ya kuendelea
kuwaburudisha mashabiki wake.
Wakati wa kibao cha ‘Yahya,’ Lulu akaibuka nyuma ya jukwaa na
akaungana na Jaydee kuimba hali ambayo iliongeza mvuto hadi wapenzi na
mashabiki kumtunza fedha binti huyo nyota wa filamu.
Baada ya wimbo huo, Lulu alisema amefurahi kuimba na Lady Jaydee kiasi cha kutamani siku moja aje kuwa mwanamuziki.
Uzinduzi huo wa filamu hiyo ya Lulu aliyocheza baada ya kutoka
mahabusu alikokuwa akishikiliwa kwa miezi kadhaa kwa tuhuma za
kusababisha kifo cha Steven Kanumba, ulishuhudiwa na wasanii kadhaa kama
Amini Mwinyimkuu, Barnaba wa THT na wale wa Bongo Movie.
No comments:
Post a Comment