MAJAMBAZI wanne waliohusika katika utekaji wa gari la Chuo Kikuu
cha Kilimo Sokoine (SUA) na kuwapora fedha waombolezaji kisha kuvunja
jeneza na kumpekua marehemu, wamehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kila
mmoja kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.
Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Singida, Flora
Ndale, mwendesha mashitaka, Sajenti wa Polisi, Godwel Laurence, alidai
kuwa Desemba 8 mwaka jana, washitakiwa kwa pamoja huko katika eneo la
Kindai barabara ya Singida-Dodoma, waliteka gari la SUA lenye namba za
usajili SU 3712 aina ya Land Cruiser hard-top lililokuwa limebeba mwili
wa marehemu, mwanafunzi wa chuo hicho kuelekea Tarime kwa maziko na
kuwapora waombolezaji fedha na mali nyingine.
Laurence alivitaja vitu vilivyoporwa kuwa ni pamoja na fedha taslimu,
kompyuta mpakato (lap top), simu ya mkononi aina ya Samsung na moderm
moja, vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya sh 8,739,000.
Aliongeza kuwa siku ya tukio, saa 7:30 usiku wa manane, washitakiwa
waliweka mawe makubwa barabarani hali iliyomlazimu dereva wa gari hilo
kusimama, na ndipo walivamiwa na kuanza kuwapiga watu marungu na fimbo
sehemu mbalimbali za miili yao na kisha kuwapora.
Alidai kuwa mkuu wa msafara huo, Makaranga Nona, pamoja na waathirika
wengine wa tukio hilo, waliweza kuwatambua washitakiwa baada ya polisi
kuendesha gwaride maalumu la utambuzi Desemba 10 mwaka jana.
Hakimu Ndale alisema upande wa mashitaka umethibitisha bila kuacha
shaka yoyote, kwamba washitakiwa wana hatia kama walivyoshitakiwa.
Alisema upande wa mashitaka umejiridhisha na mashahidi wa kesi hiyo
baada ya kuwatambua washitakiwa kwa kutumia taa za gari wakati
wakiwafanyia upekuzi huo siku ya tukio.
Pia alisema kutokana na washitakiwa kutojifunika nyuso kwa vitambaa
maalumu vinavyotumiwa na majambazi wengi kwenye uporaji, hivyo waliweza
kutambuliwa kirahisi na upande wa mashitaka.
Katika utetezi wao, washitakiwa waliiomba mahakama iwapunguzie adhabu,
kwa kuwa wengi ni vijana na wengine wana watoto wanaosoma shule, na
hivyo kuwategemea wao.
Hata hivyo, akisoma hukumu hiyo, Hakimu Ndale alisema licha ya utetezi
huo maneno yao hayana miguu ya kusimamia, na kwamba sio lazima vitu
vilivyoibwa vikutwe majumbani mwao.
“Kitendo mlichofanya ni cha kinyama na sio cha kibinadamu mbele ya
jamii, kwa hiyo mikono yangu imefungwa juu yenu, pia mmefanya makosa
ambayo adhabu yake imebainishwa wazi sio ya kupunguza bali ikiwezekana
kuongezwa.
“Mahakama hii inawahukumu kifungo cha miaka 30 jela kila mmoja ili iwe
fundisho kwenu na watu wengine wenye tabia ya kufanya vitendo vya
kinyama kama hivyo mbele ya jamii, haki ya kukata rufaa mnayo ndani ya
siku 30,” alisema.
CREDIT TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment