WAZIRI Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe, amesema Tanzania inapoteza
jumla ya dola za Marekani kati ya milioni 500 na bilioni 1.25 kwa mwaka,
kutokana na kampuni kubwa za kimataifa kukwepa kodi.
Alisema kuwa hiyo ni sawa na kusema Tanzania inapoteza dola takriban milioni mbili kila siku kwa uporaji huu,” alisema.
Kwa mujibu wa Zitto, wakati shinikizo la dunia sasa limeelekea
kumaliza tatizo la ukwepaji kodi na utoroshaji wa fedha kutoka nchi za
Kiafrika, Serikali ya Tanzania inavuta miguu.
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA) na mmoja wa
wabunge waliovalia njuga sakata la vigogo kuficha fedha katika benki za
nje, alitoa kauli hiyo katika taarifa yake aliyoisambaza kwenye vyombo
vya habari jana.
Alisema moja ya njia za serikali za nchi maskini kupata taarifa za
kampuni kubwa za kimataifa (MNCs) zinazokwepa kodi ni mfumo wa kupashana
taarifa (automatic exchange of tax information).
“Kufuatia shinikizo la nchi mbalimbali, hivi sasa nchi zinazoitwa
‘secrecy jurisdictions’ (tax havens), zimeanza kuweka sahihi makubaliano
ya kutoa taarifa. Tanzania mpaka sasa haijaweka sahihi na serikali
haijatoa taarifa yoyote kwa umma,” alisema.
Kwa mujibu wa Zitto, Ghana, Afrika Kusini na Nigeria ni nchi
zinazotegemea sana rasilimali kama Tanzania ambazo zimeweka sahihi
mkataba huu tayari.
Alisema kuwa asilimia 44 ya fedha za kigeni nchini zinatokana na mauzo
ya madini nje. Kampuni za madini ndizo zinaongoza kukwepa kodi.
“Naitaka serikali kutoa taarifa kwa nini haichukui hatua kuzuia mwanya
huu wa mapato ya umma. Serikali ichukue hatua mara moja kuhakikisha
Tanzania inaingia makubaliano ya kupashana taarifa za kikodi.
“Huu si wakati wa kuvuta miguu katika suala nyeti la umma. Badala ya
kukimbilia kutoza kodi wanyonge, tuhakikishe kampuni kubwa zinazonyonya
rasilimali zetu zinalipa kodi inayotakiwa,” alisema.
Mapema asubuhi jana, akihojiwa na kituo kimoja cha redio, Zitto
alisema sababu ya vigogo wengi kuficha fedha nje ya nchi ni ukubwa wa
kodi inayotozwa hapa nchini inayofikia asilimia 30.
Alisema kodi hiyo ni kubwa zaidi ikilinganishwa na nchi zile
wanakoficha fedha, mathalani Uswisi inatoza asilimia 0, Mauritius
asilimia 17, wakati Cayman ikitoza kati ya asilimia 0 mpaka 3.
Zitto alifafanua kuwa baada ya nchi nyingi za Ulaya na Marekani kuona
wananchi wakificha fedha zao katika nchi zao, walikaa pamoja na kuandaa
mkataba wa kuwezesha kupeana taarifa za fedha zinazokuwa zinaingizwa na
raia wa mataifa mengine.
Alisema anashangazwa kuona kwamba pamoja na nchi hizo kutoa ofa hiyo
ya kubadilishana taarifa za kikodi ni nchi nne pekee za Afrika
zilizosaini mkataba huo.
Zitto alizitaja baadhi ya benki ambazo Watanzania wengi wana fedha
kuwa ni Uingereza, Jersey, Cayman Islands, Mauritius na Dubai.
CHANZO NI TANZANIA DAIMA.
No comments:
Post a Comment