Ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Katibu wa Bunge inaonesha kuwa, muswada huo utajadiliwa kwa siku tatu mfululizo mpaka siku ya kuahirishwa kwa Bunge, Jumamosi wiki hii.
Miongoni mwa shughuli zingine zitakazofanyika ni pamoja na serikali kutoa majumuisho na ufafanuzi wa hoja za wabunge kupitia maoni yao waliyoyatoa wiki iliyopita, walipojadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2014/2015.
Sambamba na hilo, leo pia Spika anatarajiwa kutangaza majina ya wajumbe wa Kamati Teule ya Bunge ya kuchunguza migogoro baina ya wakulima na wafugaji nchini na kuwapa muda wa kazi pamoja na hadidu za rejea.
Wiki iliyopita, Bunge lilikaa kama Kamati ya Mipango kwa mujibu wa Kanuni ya 94 ya Kanuni za Bunge toleo la mwaka 2013, ili kutekeleza matakwa ya Ibara ya 63 (3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayolipa uwezo Bunge kujadili na kuishauri Serikali kuhusu mipango ya Taifa na leo ni majumuisho.
Pamoja na majumuisho hayo, pia miswada mbalimbali itajadiliwa ikiwemo Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa Mwaka 2013 utakaowasilishwa kwa mara ya pili na kujadiliwa kwa siku mbili.
Hadi jana, taarifa inaonesha kuwa, hakuna miswada mingine iliyowasilishwa na Serikali katika mkutano huu.
Hata hivyo awali ilielezwa kuwa miongoni mwa mambo yaliyotarajiwa kujadiliwa ni pamoja na Muswada Binafsi, uliowasilishwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema), ambaye anataka Sheria
ya Magazeti ya mwaka 1976, ifutwe.
Mbali na muswada huo, Bunge litaendelea na utaratibu wake wa kawaida wa vipindi vya maswali na majibu na Alhamisi wiki hii, kutakuwa na Maswali ya papo hapo kwa Waziri Mkuu.
Wiki iliyopita hakukuwa na maswali kwa Waziri Mkuu kutokana na kiongozi huyo wa shughuli za Serikali bungeni kuwa safarini nje ya nchi.
Hata hivyo, pamoja na kuwepo kwa majadiliano na maoni kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo kwa mwaka 2014/2015 yanayotarajiwa kumalizika leo, pia Bunge liliunda Kamati Teule kuchunguza migogoro ya wakulima na wafugaji na pia serikali ilitangaza bungeni kusitisha Operesheni Tokomeza Ujangili baada ya kubainika kuna upungufu wa namna ya kuitekeleza.
Taarifa zaidi zinadai kuwa, huenda Bunge likajadili Rasimu ya Mwongozo wa Kanuni za Maadili ya Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 2012 ambayo, iwapo Kamati ya Uongozi itapendekeza kufanya hivyo.
Matarajio ni kwamba, kutakuwa na majadiliano makali wakati wa kujadili Muswada wa Sheria ya Kura za Maoni wa Mwaka 2013 wiki hii, hasa ikizingatiwa kuwa Bunge la Katiba linatarajiwa kuanza hivi karibuni baada ya kumalizika Bunge hili.
CHANZO HABARI LEO
No comments:
Post a Comment