Jenerali
 Mella, Kamanda wa Jeshi la UNAMID akibadilisha mawazo na Balozi Mwinyi,
 ambapo pamoja na mambo mengine, amesema wanajeshi kutoka JWTZ ambao ni 
sehemu ya UNAMID wameendelea kuonesha weledi na kujituma kwa hali ya juu
 katika eneo la ulinzi wa amani, ulinzi wa raia na usimamiaji wa misaada
 ya kibinadamu. Akasema kutokana na mapingano ya kikabili yanajitokeza 
mara kwa mara, na kuwa sehemu kubwa ya mapigano hayo yamekuwa yakitokea 
katika maeneo zilipo kambi za wanajeshi kutoka Tanzania, wanajeshi wetu 
wamejikuta wakilazimika kutoa huduma mbalimbali zikiwamo za kuwazalisha 
wanawake waja wazito. Utoaji wa huduma hiyo ya uzazi salama nje ya 
mamlaka yao imewafanya wazazi waliojifungua kuwapatia majina ya 
kitanzania watoto wao, kama shukrani yao kwa madaktari hao wa kitanzania
 kwa kuokoa maisha yao na ya watoto wao. Kushoto kwa Jenerali Mella, ni 
Luteni Kanali, Wilbert Ibuge, Mwambata Jeshi katika Uwakilishi wa Kudumu
Luteni
 Jenerali Paul Mella, Kamanda wa Jeshi la Mseto la Umoja wa Afrika na 
Umoja wa Mataifa katika Darfur ( UNAMID) akisisitiza jambo wakati wa 
mazungumzo yake na Balozi Ramadhan Mwinyi, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa
 Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa ( hayupo 
pichani). Jenerali Mella alifika katika Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania
 kufuatia ziara yake ya kikazi ya siku tatu katika Umoja wa Mataifa 
ambapo alikuwa na mazungumzo na Wakuu mbalimbali wa UN. Akielezea 
tathmini yake ya miezi nane kama Kamanda wa UNAMID Jenerali Mella 
anasema njia pekee ya kupatikana kwa amani ya kudumu katika jimbo la 
Darfur ni kwa pande zinazopingana kukaa katika meza ya mazungumzo na 
kumaliza tofauti zao.
Na Mwandishi Maalum
Kamanda
 wa Jeshi la Mseto la Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa katika Darfur (
 UNAMID) Luteni Jenerali Paul Mella, amesema, mazungumzo 
yatakayozihusisha pande zote zinazopingana katika mgogoro na machafuko 
yanayoendelea katika Jimbo la Darfur ndiyo suluhu pekee inayoweza 
kurejesha hali ya Amani, usalama na utulivu katika jimbo hilo.
Jenerali
 Mella, ameyasema hayo wakati alipokuwa akibadilishana mawazo na Balozi 
Ramadhani Mwinyi, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa 
Tanzania katika Umoja wa Mataifa, wakati Jenerali Mella alipoutembelea 
Uwakilishi wa Kudumu.
Kamanda
 wa Jeshi la UNAMID alikuwa hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa kwa 
ziara ya kikazi ya siku tatu, ambapo alikutana na kufanya mazungumzo na 
Viongozi mbalimbali wa Umoja wa Mataifa.
“Katika
 kipindi changu za miezi nane sasa kama kamanda wa UNAMID yapo mambo 
mengi ambayo nimejifunza zikiwamo pia changamoto mbalimbali katika eneo 
zima la ulinzi wa Amani katika Jimbo la Darfur. Kubwa la msingi ambalo 
nimejifunza, ni kwamba, Amani ya kudumu haiwezi kurejea katika jimbo la 
Darfur kama pande zote zinazopingana hazitaweza kukaa katika meza moja 
na kufanya mazungumzo” anasema Jenerali Mella.
Na 
kuongeza “ kwa tathmini yangu , wanajeshi wanaounda UNAMID wapo pale 
kulinda Amani, kutoa ulinzi kwa wananchi na kusaidia usambazaji wa 
misaada ya kibinadamu. Lakini kwa kweli, hakuna Amani ya kulinda, kwa 
sababu moja kubwa, nayo ni kwamba pande zinazopingana hazijafikia 
makubaliano ya kusitisha mapigano na kurejea katika meza ya mazungumzo.”
Akielezea
 zaidi tathmini yake katika kipindi hicho ya miezi nane ambapo anaongoza
 zaidi ya walinzi wa Amani (wanajeshi)14,379 wanaounda UNAMID. Jenerali 
Mella, anaeleza kwamba, tangu achukue uongozi huo, kumekuwapo na 
mabadiliko katika mwenendo mzima wa mapigano katika jimbo hilo.
“ 
Changamoto kubwa niliyokumbana nayo ni kuwa katika miezi hiyo nane ya 
uongozi wangu, mwenendo mzima wa machafuko au mapingano umebadilika na 
kujikita zaidi katika mapigano ya kikabila” anabainisha na kuongeza.
“Mapigano
 hayo ya kikabili na ambayo chimbuko lake ni kugombea raslimali zikiwamo
 dhahabu mafuta na malisho, yamepelekea kuwapo kwa wimbi kubwa la 
wakimbizi wa ndani.
Jenerali
 Mella anasema, sehemu kubwa ya mapingano hiyo baina ya makabila 
yalikuwa yanatokea karibu na maeneo zilipo kambi zetu kwa maana ya 
wanajeshi kutoka Jeshi la wananchi wa Tanzania ( JWTZ). Ninafarijika 
sana kueleza kwamba wanajeshi wetu wameonyesha weledi na uhodari wa hali
 ya juu kwanza kwa kutoa ulinzi kwa raia waliokuwa wakikimbia machafuko 
na pili kuwapatia misaada ya kibinadamu zikiwamo huduma za afya”.
“Ni 
katika kipindi hicho cha mapigano ambapo licha ya utoaji wa huduma za 
kibinadamu kwa wakimbizi hao, walinzi wetu wa Amani ( JWTZ), walijikuta 
wakilazimika kutoa huduma za dharura kwa akina mama wajawazito zaidi ya 
saba waliojifungua salama watoto wao katika kambi zetu”.
“ 
Huduma hii ya kuwasaidia akina mama wajawazito kujifungua salama watoto 
wao, kuliwafanya wazazi wale kuwapa watoto wao majina ya kitanzania kama
 shukrani yao kwa msaada na huduma nzuri waliyopatiwa na madaktari wa 
kitanzania katika kipindi hicho kigumu. Kuna watoto wenye majina ya 
kitanzania” anasema Jenerali Mella kwa furaha.
Kwa 
upande wake, Balozi Mwinyi ameshukuru Kamanda wa Jeshi la UNAMID kwa 
kutenga muda wake na kufika Uwakilishi wa Kudumu. Akashukuru pia kwa 
maelezo yake ya kina kuhusu hali ilivyo katika jimbo hilo la Darfur na 
mchango mzima wa walinzi wa Amani.
Jamhuri
 ya Muungano wa Tanzania, ina kikosi UNAMID kinacho kalia maeneo matatu 
ambayo ni Khor Abeche, Menawashe na Shangil Tobaya.
Tanzania inakuwa nchi ya tatu kongoza UNAMID , nchi nyingine ambazo zimewahi kuongoza ni Nigeria na Rwanda.
No comments:
Post a Comment