Makamu Mkuu wa Chuo cha International Medical and Technological University (IMTU), Profesa PV Prabhak Rao (mwenye koti la blue) na viongozi wengine wakisindikizwa na polisi kuingia kwenye Kituo cha Oysterbay, Dar es Salaam jana, kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na upatikanaji wa viungo vya binadamu eneo la Mpigi Bunju. Picha na Rafael Lubava
Dar es Salaam.
Wakati ikibainika kuwa viungo vya miili ya binadamu vilivyookotwa juzi katika Bonde la Mto Mpiji nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam vilitoka katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU), jana Jeshi la Polisi liliwatia nguvuni watumishi wanane wa chuo hicho kuhusiana na sakata hilo.
Kukamatwa kwa watumishi hao kumeelezwa na Kamanda
wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kuwa ni baada ya
uchunguzi wa awali kubaini kuwa viungo hivyo kwa mara ya mwisho
vilikuwa katika maabara ya IMTU.
Alisema tukio hilo lilitokea juzi jioni eneo la
Bonde la Mbweni Mpiji ambako iligundulika mifuko ya plastiki 85 yenye
mabaki ya viungo vya binadamu.
Kutokana na tukio hilo, Polisi imeunda jopo la
wapelelezi saba likiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu, Jafari
Mohamed kusaidiana na daktari wa jeshi hilo kufanya uchunguzi wa miili
hiyo.
“Katika uchunguzi wetu tulibaini kuwa hivyo viungo
vya binadamu vilitolewa katika Chuo cha IMTU na kusindikizwa na
mfanyakazi wa ngazi ya juu kwa ajili ya kutupwa eneo la Bonde la Mbweni
Mpiji,” alisema Kova.
Alisema mifuko hiyo ilikuwa myeusi ikiwa na viungo
vya aina mbalimbali vikiwamo vichwa, miguu, mikono, moyo, mapafu, vifua
na mifupa ya aina mbalimbali.
“Viungo hivyo havikuwa na harufu wala uvundo wa aina yoyote na vilionekana vimekaushwa na kukakamaa,” alisema.
Alisema katika eneo hilo walikuta vifaa
vinavyotumika hospitali kama glovu, nguo maalumu (apron) 20 na karatasi
mbili zenye maswali ya kujibu.
Kova alisema viungo hivyo vilichukuliwa na kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Alisema jeshi hilo limefungua jalada la uchunguzi
ili kujua sheria gani imevunjwa na kwa nini viungo hivyo vilitupwa hapo
na kwa nini wasitumie utaratibu mzuri wa kuhifadhi na kwamba endapo kuna
makosa ya kisheria, hatua zitachukuliwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa
Mashtaka (DPP).
Muhimbili wapokea mabaki
Meneja Uhusiano wa MNH, Aminiel Aligaesha alisema
jana kuwa hospitali hiyo imepokea vifurushi 40 vyenye mabaki ya miili ya
binadamu na kuhifadhiwa wakisubiri maelekezo ya polisi... “Hili ni
suala la polisi, ninachoweza kusema ni kweli tumepokea vifurushi hivyo
jana (juzi) usiku.”
IMTU yakiri kuhusika
Wakati Kova akisema hayo, uongozi wa IMTU ulikiri
kuhusika na mabaki ya miili hiyo yaliyotupwa katika mto huo usiku wa
kuamkia Jumapili iliyopita.
Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho, Dk Fariji Mtango
alisema jana kwamba anaamini miili hiyo inaweza kuwa ni ile iliyotoka
katika chuo hicho, ambayo imekuwa ikifanyiwa mazoezi na wanafunzi kwa
kuwa walihitaji kuiteketeza na walishatoa agizo hilo.
Alisema walitoa agizo kwamba mabaki hayo yapelekwe
Muhimbili kwa mujibu wa utaratibu wao kwa kuwa hayakuwa na matumizi
tena, kwa kuwa ndiyo sehemu yenye uwezo wa kuyateketeza na kutoa jukumu
hilo kwa mmoja wa wakufunzi wa chuo hicho ambaye jana alikuwa safarini.
“Sasa zaidi hatujui kilichoendelea lakini
tulipoangalia jana (Jumatatu) tulikuta sehemu yalipohifadhiwa
imesafishwa, hivyo inawezekana ni sehemu ya vile vilivyoondolewa hapa.
Hatukutarajia kwamba vingetupwa katika eneo lisilokuwa sahihi kama
ilivyofanyika,” alisema.
Dk Mtango alisema hiyo ilikuwa moja ya hatua za
kupisha wakaguzi ambao walitarajiwa kukuta maeneo yote ya kufundishia
yakiwa katika hali ya usafi na unadhifu.
“Hawa wakaguzi wanapokuja wanatakiwa waone vitu
vyote vikiwa sawa. Hata kama wangeona hayo mabaki ya miili ya binadamu
isingekuwa tatizo, bahati nzuri wamekuja jana na wamefanya kazi yao
vizuri,” alisema.
Muda mfupi baada ya kutolewa kauli hiyo, viongozi
tisa wa chuo hicho na walinzi wawili walikamatwa mnamo saa 7.30 mchana
na kupelekwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay ambako wanashikiliwa,
lakini baadaye Kova alisema waliokamatwa ni wanane.
Jana mchana eneo la chuo cha IMTU lilikuwa chini
ya ulinzi mkali wa polisi waliotanda kuanzia getini, mapokezi na kwenye
bustani za chuo hicho na wengine waliovalia sare maarufu kama ‘tigo’
ambao walikuwa wakishika doria mbele ya chuo hicho.
Hatua kuchukuliwa
Dk Mtango alisema uongozi wa chuo hicho
umeshtushwa na kutupwa kwa mabaki hayo katika utaratibu usiokubalika na
utafanya uchunguzi na kuchukua hatua kwa wote waliohusika.
“Tunaanza na huyu ambaye tulimpa hili jukumu. Yeye
ndiye aliyetakiwa kusimamia na anaujua wazi utaratibu wetu. Kwa sasa
hajafika hapa na hata simu yake haipatikani. Tunaarifiwa kwamba
amekwenda Zanzibar,” alisema.
Jinsi ilivyotokea
Juzi jioni, ilitokea taharuki baada ya wananchi
kubaini viungo hivyo na taarifa kuanza kusambaa katika mitandao ya
kijamii na baadaye vyombo vya habari na hadi jana mjadala kuhusu suala
hilo ulikuwa mzito na wananchi wakihoji miili hiyo ni ya watu gani,
imetoka wapi na imetupwa na watu gani.
Shuhuda wa tukio hilo, Mariam Nkumba alisema mara
ya kwanza aliona mifuko yenye viungo hivyo Jumapili alipokwenda kuponda
kokoto katika eneo hilo lakini hakubaini kulikuwa na nini.
Siku hiyo, Nkumba alisema aliondoka katika eneo
hilo saa 12 jioni bila kujua nini kilikuwa ndani ya mifuko hiyo na siku
iliyofuata (Jumatatu), alikwenda kuchukua mfuko mmoja ili ahifadhie
kokoto zake, ndipo aliposhtuka kuona viungo vya binadamu.
“Mifuko ilikuwa mingi kweli, yote ilikuwa imejaa
viungo vya binadamu. Mpaka sasa sijala na sina hamu ya kula. Ukiiona ile
miili huwezi kula chakula,” alisema.
Mfanyakazi wa Kampuni ya Ujenzi ya Skol iliyopo
karibu na eneo hilo, Supery Kaijunga alisema mara alipopata taarifa
kutoka kwa Nkumba alianza kutoa taarifa kwa wananchi wengine ili kwa
pamoja wajue la kufanya.
Baadaye walitoa taarifa polisi ambao walifika saa mbili usiku na kukusanya mabaki yote na kuondoka nayo.
Hata hivyo, Kaijunga alieleza wasiwasi wake kuhusu wingi wa miili hiyo na kuhoji walikuwa watu gani na walitoka maeneo gani.
“Tukio hili siyo la kawaida na halijawahi kutokea
huku kwetu. Tunakuwa na wasiwasi sana labda nasi maisha yetu
yatachukuliwa kama hawa; polisi wafanye uchunguzi wa kina kubaini ukweli
wake,” alisema Kaijunga.
Imeandikwa na Andrew Msechu, Peter Elias na Pamela Chilongola wa Mwananchi.
No comments:
Post a Comment