Wakati vyombo vya juu vya baadhi ya vyama vya siasa vikiwa vimeanza hatua za mwisho za kupitisha wagombea wa ubunge na udiwani tayari kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, hadi juzi wabunge 51 walikuwa wameanguka kwenye kura za maoni za ndani ya vyama vyao.
Idadi hiyo ni takriban asilimia 14 ya wabunge 357 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, inayojumuisha waliochaguliwa na wananchi na wa viti maalumu, ambao waliamua kwenda kupambana majimboni.
Miongoni mwa walioanguka ni mawaziri wa Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambao walikuwa wakitetea viti vyao majimboni.
Kati ya wabunge hao walioanguka, wawili wanatoka Chadema, wanne CUF na wengine 45 waliosalia wanatoka CCM.
Matumaini pekee yaliyosalia kwa wabunge hao ambao baadhi yao wamekata rufaa kupinga matokeo ya kura za maoni, ni huruma za vikao hivyo ambavyo vinaweza kubadili matokeo ya baadhi ya majimbo, hasa ambayo taratibu zilikiukwa na ushahidi wa kuwapo matumizi ya rushwa.
Wakati wabunge walioanguka Chadema wanasubiri kwa hamu kikao cha Kamati Kuu kilichoanza juzi kupitia majina hayo, wa CCM wanasubiri mfululizo wa vikao vinavyoanza leo hadi Agosti 13, wakati mchakato kupitisha wagombea wa NCCR-Mageuzi bado.
Kwa wabunge wa CUF, hakuna matumaini kutokana na vikao vya juu vya chama hicho kukamilisha kazi yake hivi karibuni.
Mbali na walioanguka, wabunge waliopita katika kura za maoni lakini vyama vyao vinaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), nao watalazimika kusubiri hadi vyombo hivyo vya mchujo vitakapomaliza kazi, kujua kama wamepita.
Hiyo inatokana na makubaliano ndani ya umoja huo ya kusimamisha mgombea mmoja atakayeungwa mkono na vyama vyote.
Kwa mujibu wa makubaliano ya vyama hivyo vinne; Chadema, CUF, NLD na NCCR - Mageuzi- kinachooonekana kina nguvu kwenye jimbo fulani ndicho mgombea wake ataachiwa kupeperusha bendera ya umoja huo, jambo ambalo vyama hivyo vilisema vimekamilisha kazi ya mgawanyo kwa asilimia 95.
Wakati Chadema, CUF, NCCR na NLD wakisubiri utekelezwa wa makubaliano hayo, wabunge wa CCM watakuwa njiapanda baada ya chama hicho kueleza kuwa hakitarudia makosa ya mwaka 2010 ya kupingana na maoni ya wanachama kwa kutengua matokeo ya kura za maoni.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Jamidu Katima alisema kuanguka kwa wabunge hao kunatokana na wengi wao kutoonekana majimboni baada ya kupewa dhamana ya kuongoza wananchi.
“Kama kiongozi umepewa dhamana, lakini huonekani jimboni basi ni dhahiri wananchi watakukataa. Wakikuona unachukua fomu watakushangaa lakini ujue watakukataa kwa sababu huwatatulii kero zao kama ulivyoahidi awali.”
Profesa Katima alisema kwa sasa Watanzania wameamka, hivyo ni vigumu kudanganyika na kwamba kama kiongozi hatumii vyema dhamana aliyopewa, wananchi watamuacha apumzike kwa amani.
Maoni kama hayo yalitolewa na mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo ambaye alisema zipo sababu chekwa za baadhi ya mawaziri kushindwa kwenye kura za maoni, mojawapo ikiwa ni makundi na kushindwa kutimiza ahadi.
Kujaribu mtu mwingine
Dk Makulilo alisema ni rahisi kwa wananchi kuacha kumchagua kiongozi baada ya kuona hajatimiza kile alichoahidi hivyo wakaona wajaribu kiongozi mwingine pengine atawatatulia kero zao.
Kuhusu kuanguka kwa wanasiasa nguli wa CCM, mhadhiri huyo alisema sababu nyingine ni siasa za makundi ambako kundi moja tu linaweza kufanya juhudi ili mwingine ashindwe.
“Sasa hivi tunazungumzia mtu kuanguka katika chama chake, kwa hiyo siasa za makundi ndani ya chama hicho inaweza kusababisha kuanguka katika kura za maoni,” alisema.
Sababu nyingine aliyoitaja Dk Makulilo ni wimbi la vijana na kuwa inawezekana wananchi wanahamia kwa wanasiasa vijana zaidi baada ya kuona wengine amekaa madarakani kwa muda mrefu.
Pia, aliitaja rushwa kuwa miongoni mwa sababu za kuanguka kwani inawezekana kuwa mgombea mwenzake ametoa fedha au yeye ametoa, lakini mwingine ametoa nyingi zaidi.
“Nadhani umeona jinsi ambavyo Takukuru wamekamata wagombea wengi kwa tuhuma za rushwa kwa hiyo hapana shaka kuwa suala la rushwa lilikuwepo,” alisema.
Utafiti wa Twaweza
Idadi ya wagombea hao walioanguka katika hatua ya awali inaashiria kuanza kutimia kwa matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi ya Twaweza mwishoni mwa mwaka jana ambao ulionyesha kuwa nusu ya wabunge wataanguka kwenye kura za maoni.
Kwa mujibu wa utafiti huo uliotangazwa Novemba 12, 2014, kuanguka kwa wabunge hao kutatokana na kushindwa kutekeleza ahadi zao. Asilimia 47 ya wananchi walioulizwa iwapo watampigia tena kura mbunge wao, walisema “hapana” huku asilimia kama hiyo ikisema “ndiyo”.
Utafiti huo ulieleza kuwa ahadi nyingi zilizotolewa na wabunge kwenye mikutano ya kampeni wakati wa uchaguzi hazijatekelezwa na kwamba asilimia 78 ya wananchi bado wanazikumbuka.
CCM kutorudia makosa
Wakati utafiti wa Twaweza ukizungumzia kutotimizwa kwa ahadi, wabunge waliopita kura za maoni watakuwa wakijifariji na matamshi ya viongozi wao kuwa majina yao hayatakatwa kama ilivyokuwa mwaka 2010.
Akihutubia kwenye mkutano wa hadhara mjini Iringa Oktoba mwaka jana, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema chama hicho hakitarudia makosa ya kuengua majina ya wagombea wanaopitishwa na wanachama kwenye kura za maoni baada ya Frederick Mwakalebela kuenguliwa na Halmashauri Kuu kugombea ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini na baadaye Mchungaji Peter Msigwa wa Chadema akatwaa jimbo hilo.
No comments:
Post a Comment