Mkurugenzi
Mtendaji wa zamani wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), David Mattaka
na wenzake wawili wamepandishwa kizimbani wakikabiliwa na mashtaka sita
yakiwamo ya matumizi mabaya ya madaraka, kughushi na kuisababishia
hasara Serikali kupitia ukodishaji wa ndege.
Wakili
Mkuu wa Serikali, Timon Vitalis akishirikiana na mawakili wa Takukuru,
Joseph Kiula na Stanley Luoga waliwataja washtakiwa wengine
wanaokabiliwa na kesi hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage
kuwa ni Ofisa Mtendaji Mkuu Mstaafu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi
ya Umma (PPRA), Ramadhan Mlinga na Mwanasheria wa mamlaka hiyo, Bertha
Soka.
Wakili
Vitalis alidai kuwa Oktoba 9, 2007 katika ofisi za ATCL zilizopo
wilayani Ilala, Mattaka alitumia vibaya madaraka kwa kutia saini mkataba
wa ukodishaji wa ndege A320-214 iliyotengenezwa kwa namba 630 baina ya
Wallis Trading Inc na ATCL.