NI kweli ajali haina kinga! Nyota wa nyimbo za Injili Bongo, Bahati Lusako Bukuku ameumia mgongo na maeneo kadhaa ya mwili (nusu kifo) kiasi cha kushindwa kukaa, kusimama wala kutembea kufuatia ajali mbaya ya gari iliyotokea kwenye eneo la Ranchi ya Narco wilayani Kongwa, Dodoma saa tisa usiku wa kuamkia Jumamosi, Ijumaa Wikienda lina undani wa mkasa mzima.
Kwa mujibu wa chanzo makini, katika ajali hiyo ambayo Bahati alikuwa akienda Kahama, Shinyanga kwenye mkutano wa Injili, dereva wa gari alilokuwa akisafiria aina ya Toyota Nadia lenye namba za usajili IT 7945, Edison Mwakabungu ‘Eddy’ (31) aliumia sana kwenye vidole vya miguu na hawezi kutembea.
Wengine waliokuwemo kwenye ajali hiyo ni wacheza shoo wa Bahati, Frank Muha (20) na mwenzake ambaye jina lake halikupatikana mara moja.
ILIKUWAJE?
Habari zilidai kuwa gari hilo halikuwa na matatizo hivyo kumfanya dereva wake kukanyaga mafuta kwa wastani wa kilometa 120 kwa saa.“Sasa walipofika eneo la Kibaigwa, walikutana na lori likitokea Dodoma kwenda Morogoro, wakavaana kwa mbele. Nadia likatoka barabarani hadi porini likiwa limeharibika kuanzia kwenye shoo ya mbele, injini na siti za mbele halafu lori hilo likakimbia.
“Nadia ilipotulia, Bahati alijikuta hawezi kufanya chochote, dereva wake naye ameumia kwenye vidole vya miguu. Wale wawili waliokuwa siti ya nyuma, wote walijeruhiwa lakini mmoja si sana. Ilibidi yeye abaki pale na gari ili majeruhi wengine wakimbizwe Hospitali ya Wilaya ya Kongwa, Dodoma kwa matibabu,” kilisema chanzo hicho.
Gari alilopata nalo ajali mwimbaji wa nyimbo za Injili Bongo, Bahati Bukuku aina ya Toyota Nadia lenye namba za usajili IT 7945.
HABARI NYINGINEHabari ambazo hazijathibitishwa na dereva wa Bahati zilisema kuwa, wakati gari hilo linakaribiana na lori, dereva wa lori aliwasha taa ‘full’ (mwanga mkali) hivyo kumfanya dereva huyo kushindwa kuona mbele vizuri, jambo ambalo ni kinyume na sheria za usalama barabarani.
ROSE MUHANDO, JENNIFER MGENDI WAFUNGA SAFARI
Ilidaiwa kuwa usiku huohuo, waimba Injili mahiri Tanzania, Rose Muhando na Jennifer Mgendi walipata taarifa za ajali hiyo na kufunga safari ya kwenda Kongwa kuangalia namna ya kuwahamishia majeruhi hao kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar.
ROSE MUHANDO
Rose Muhando alipotafutwa kwa simu juzi mchana na kuulizwa kuhusu kusafiri kwenda Kongwa, alikiri na kusema wameshafika na Jennifer Mgendi.
“Ndiyo tupo kwenye hekaheka ndugu yangu. Tuna dhamira ya kuwachukua majeruhi kuwapeleka Muhimbili kwa matibabu zaidi,” alisema Rose.
JENNIFER MGENDI
Yeye alipopatikana alisema alishtushwa na simu asiyoijua usiku mnene na kuambiwa shoga yake huyo amepata ajali mbaya ya gari.“Kitu cha kwanza niliuliza hali yake, nikaambiwa ameumia mgongo, dereva wake mguu. Ndiyo nikaanza kuwataarifu wadau wengine na mimi kujiandaa kwa safari kutoka Dar kuja Kongwa usiku huohuo. Kwa kweli ameumia,” alisema Mgendi ambaye ni rafiki mkubwa wa Bahati.
Naye Katibu wa Chama cha Waimba Injili Tanzania, Stella Joel alipozungumza na gazeti hili juzi, alikiri waimba injili hao kuondoka Dar es Salaam kuelekea Dodoma kumpa msaada mwenzao.
BAHATI BUKUKU AZUNGUMZA KWA TABU
Alfajiri ya juzi, mwandishi wa habari hizi alimpigia simu Bahati na kuongea naye kuhusu ajali hiyo ambapo huku akisikika kama anayepata tabu kwa maumivu, alisema:
“Ni kweli tumepata ajali, nimeumia mgongoni, dereva ameumia mguu. Namshukuru Mungu. Sijui nini kilitokea, nilishtukia kuona gari kubwa mbele yetu likituvaa, mara nikashtukia tuko porini. Lakini kabla ya safari Dar tulifanya maombi makubwa, najua Mungu ametunusuru na kifo kibaya,” alisema Bahati.
Mwandishi: “Unadhani nani alikuwa na kosa kati ya dereva wako na wa lori?”Bahati: “Sijui chochote. Halafu najisikia vibaya sana, tuwasiliane baadaye kaka ‘angu.”
UZOEFU WA DEREVA
Habari zinasema kwamba, Eddy ni dereva wa miaka mingi. Mbali na jijini Dar, pia amekuwa akiendesha magari kwenda nje ya Tanzania kama Burundi na Rwanda na katika ajali hiyo alikuwa akienda nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), hivyo ana uzoefu wa safari za usiku.
WATU WA INJILI NA AJALI ZA DODOMA
Kumbukumbu zinaonesha kuwa hii si mara ya kwanza kuripotiwa kwa ajali za magari mkoani Dodoma zikiwahusisha watu wa tasnia Injili Bongo.
Aprili, mwaka huu, Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotion, Alex Msama alipata ajali mbaya ya gari kwa kugongana na mwendesha bodaboda.Ajali hiyo ilitokea maeneo ya Ipagala Mwisho, kilomita chache kabla ya kufika mjini Dodoma. Msama alikuwa kwenye gari lake aina ya Toyota Mark II GX 100.
Katika ajali hiyo, Msama na mwendesha bodaboda huyo waliumia sehemu mbalimbali za mwili na kukimbizwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu.
Kabla ajali ya Msama haijapoa, Mei, mwaka huu, Edson Mwasabwite naye alipata ajali kwenye Barabara Kuu ya Dodoma–Morogoro. Alikuwa akitoka Dodoma kurudi Dar. Alinusurika.
CHANZO: GLOBAL PUBLISHERS
No comments:
Post a Comment